BALOZI WA KOREA AVUTIWA NA BIDHAA ZINAZOZALISHWA NA VETA,AAHIDI USHIRIKIANO
Na Mussa Augustine.
Ziara ya Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Eunje Anh katika banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), imefungua matarajio mapya ya ushirikiano katika mafunzo, uhamishaji wa teknolojia na biashara baada ya kuvutiwa na ubunifu na bidhaa zinazozalishwa na taasisi hiyo.
Meneja wa kampuni tanzu ya VETA, Ujuzi Corporate Company Limited, Mhandisi Marco Kapinga, amesema ujio wa balozi huyo ni hatua muhimu kutokana na ushirikiano ambao tayari upo kati ya VETA na Korea katika maeneo mbalimbali.
Kapinga alisema ushirikiano huo unahusisha mafunzo pamoja na uhamishaji wa teknolojia unaolenga kuendelea kuimarisha uwezo wa uzalishaji na ubunifu nchini.
"Tumefurahishwa sana na ujio wa Balozi wa Korea Kusini katika banda letu kwa sababu tuna mashirikiano mbalimbali na Korea, hususan kwenye mafunzo na pia tunashirikiana katika kuhamisha teknolojia ili tuweze kuendelea zaidi," alisema Kapinga.
Alisema balozi huyo alivutiwa na bidhaa mbalimbali zilizokuwa zikionyeshwa, hususan bidhaa zinazotokana na mazao ya baharini pamoja na bidhaa nyingine zilizozalishwa na VETA.
Kwa mujibu wa Kapinga, balozi huyo alionesha nia ya kuendelea kushirikiana na VETA katika hatua za baadaye, ikiwemo kuangalia fursa za biashara zinazohusisha bidhaa hizo.
"Amefurahishwa sana na uzalishaji aliouona, hususan vifaa vinavyotokana na mazao ya baharini pamoja na bidhaa zake zote. Amezipenda sana na tunaamini kutakuwa na mashirikiano ya baadaye kwenye biashara," alisema.
Aidha, alisema balozi huyo alivutiwa pia na bidhaa za thamani zinazotokana na mti wa mtiki, akieleza kuwa zimeonyesha uwezo wa Tanzania kuzalisha bidhaa zinazoweza kuingia katika soko la kimataifa.
"Ameona kwamba tunaweza kuzalisha vitu ambavyo vinaweza kuingia kwenye soko la kimataifa," alisema Kapinga.
Katika ziara hiyo, balozi huyo pia alitembelea eneo la vijana wenye mahitaji maalum na kushuhudia kazi wanazozifanya, jambo lililomvutia kutokana na uwezo wao wa kujitegemea kupitia elimu ya ufundi.
Kapinga alisema balozi huyo ameahidi kuangalia namna ya kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza elimu kwa watu wenye mahitaji maalum.
"Ameona kwamba licha ya hali walizonazo, wana uwezo wa kujiendesha maisha yao wenyewe, na ameahidi kuangalia namna ya kushirikiana nasi katika kuendeleza elimu kwa watu wenye mahitaji maalum," alisema.
Ameongeza kuwa ubunifu uliooneshwa na VETA katika sekta mbalimbali ulimvutia balozi huyo, akitaja uzalishaji wa viatu, nguo pamoja na bidhaa za chakula zinazotumika katika sekta ya hoteli, ikiwemo biskuti na bidhaa nyingine.
Kapinga alisema mwishoni mwa ziara hiyo balozi huyo alichukua mawasiliano ya VETA kwa ajili ya kuendelea na hatua za ziada zitakazowezesha pande hizo mbili kuimarisha ushirikiano kupitia Ubalozi wa Korea.

No comments
Post a Comment