WATANZANIA WAASWA KUEPUKA WANASIASA NA WANAHARAKATI WANAOCHOCHEA VURUGU
Watanzania wameaswa kuacha kusikiliza wanaharakati na wanasiasa wanaochochea vurugu na uvunjifu wa amani nchini, kwa kuwa watu hao hawana nia njema kwa taifa.
Rai hiyo ilitolewa leo, Juni 4, 2026, jijini Dar es Salaam na mwanafalsafa wa Pan-Afrika kutoka Zimbabwe, Dk. Joshua Maponga, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliohusu uzinduzi wa makala inayozungumzia matukio yaliyojitokeza kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.Makala hiyo imeandaliwa na kampuni ya African Spear Head Media.
Dk. Maponga alisema kuwa baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yamekuwa yakipokea fedha kutoka mataifa ya nje kwa lengo la kuhamasisha vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili na amani ya nchi, ikiwemo vurugu na migawanyiko kati ya wananchi na viongozi wao.
Alisema hali hiyo ni hatari kwa ustawi na usalama wa taifa, hivyo akashauri Serikali kuchukua hatua za kufanya uhakiki wa mashirika hayo ili kubaini vyanzo vya fedha wanazopata na namna zinavyotumika.
Aidha, alieleza kuwa watu wanaochochea vurugu mara nyingi huishi nje ya nchi katika mazingira mazuri, huku wananchi wanaoshiriki machafuko hayo wakikabiliwa na madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha, mali na makazi yao.
Dk. Maponga pia aliwataka waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za maandamano yasiyo ya amani na vurugu, akisisitiza kuwa matukio hayo yanaweza kuathiri maendeleo na rasilimali za taifa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa African Spear Head Media, David Hundeyin, alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi muhimu kiuchumi barani Afrika kutokana na nafasi yake ya kimkakati, hususan kupitia Bandari ya Dar es Salaam inayotumiwa na mataifa mbalimbali katika shughuli za biashara na uchumi.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kulinda amani na rasilimali za nchi yao, kwani machafuko yanaweza kusababisha mdororo mkubwa wa uchumi na kuathiri maendeleo ya taifa.
“Vurugu na mauaji yaliyotokea Oktoba 29, 2025 yalikuwa na athari kubwa kwa jamii. Hata hivyo, bado kuna baadhi ya watu wanaoendelea kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu.Wananchi wanapaswa kuwa makini na watu wa aina hiyo kwa kuwa hawana nia njema kwa taifa lao,” alisema Hundeyin.

No comments
Post a Comment