WATUMISHI 12 WA MANISPAA YA KIGAMBONI WAFIKISHWA MAHAKAMANI
Na Mussa Augustine
Watumishi 12 wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na Ofisi ya Rais TAMISEMI wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za wizi na ubadhilifu wa fedha kiasi cha shilingi 169,617,520, maarufu kama fedha za bakaa.
Taarifa hiyo imetolewa leo, Juni 2, 2026, jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, Francis Luena, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026.
Luena amesema uchunguzi ulifanyika kwa mujibu wa sheria na kwamba Septemba 2, 2025, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa ya kuendesha genge la uhalifu, uchepuzi, ubadhilifu, utakatishaji fedha na kuisababishia hasara Serikali. Makosa hayo ni kinyume cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Na. 200, Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 329, na Sheria ya Utakatishaji Fedha Na. 423.
“Waliofikishwa mahakamani ambao ni watumishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na vyeo vyao kwenye mabano ni Annie Nyabugumba (Afisa Hesabu Mwandamizi), Tumsifu Christopher Kachira (Afisa Hesabu Mwandamizi Daraja la I) na Aidan Zabron Mponzi (Afisa Hesabu Daraja la I),” amesema Luena.
Ameongeza kuwa watumishi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ni Jonathan Stanley Manguli (aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha MUSE), Godfrey James Martiny (Mweka Hazina), Juvenalis Babilas Mauna (Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Taka na Usafi wa Mazingira), Josephat Mutembei (Mhandisi), Bibiana Romanus Mdete (Mtunza Bohari) na Henry Herman Rugayi (Afisa Ugavi).
Wengine watatu ni wafanyabiashara ambao ni Hamis Kashinje Manfred (Mkurugenzi Mtendaji wa Konya Investment Co. Ltd), Paul Sam Mwakyusa (Mmiliki wa Mbogholo Investment Co. Ltd) na Godwin Adamson Cheyo (Mmiliki wa Macheye TZ Investment).
Hata hivyo, amefafanua kuwa kufikia Machi 2026, washtakiwa watatu ambao ni Juvenalis Babilas Mauna, Josephat Mutembei na Hamis Kashinje Manfred walikiri makosa yao kupitia makubaliano (plea bargain) na wamerejesha jumla ya shilingi milioni 87 pamoja na kulipa faini ya shilingi milioni 3.5.
“Mshtakiwa Juvenalis Babilas Mauna amerejesha shilingi milioni 27 na kulipa faini ya shilingi milioni 2. Hamis Kashinje Manfred amerejesha shilingi milioni 40 na kulipa faini ya shilingi milioni 1.5, huku Josephat Mutembei akirejesha shilingi milioni 20. Washtakiwa tisa waliobakia, shauri lao linaendelea mahakamani,” amesema.


No comments
Post a Comment