TAKUKURU TEMEKE YAREJESHA SHILINGI.370,000 KWA MADEREVA BAJAJI 40
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanikiwa kurejesha shilingi 370,000 kwa madereva bajaji 40 wa kituo cha Kibada, Halmashauri ya Kigamboni, Jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo, Juni 2, 2026, Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Francis Luena, wakati akizungumza na waandishi wa habari. Alibainisha kuwa madereva hao walitozwa fedha hizo kwa njia isiyo halali wakidaiwa kulipia stika za maegesho.
“Uchunguzi uliofanyika kwa kushirikiana na uongozi wa madereva na vyombo vya dola ulibaini udanganyifu huo, na hatua zilichukuliwa. Fedha zimerejeshwa kwa wahusika pamoja na kuimarisha utulivu na amani katika kituo hicho,” amesema.
Aidha, katika robo ya Januari hadi Machi, TAKUKURU Mkoa wa Temeke imepokea malalamiko 68, ikiwa ni ongezeko la asilimia 41.7 ikilinganishwa na robo iliyopita.
“Hali hii inaashiria kuimarika kwa imani ya wananchi na utayari wa kuripoti vitendo vya rushwa,” amesema Luena.
Ameongeza kuwa asilimia 76.5 ya malalamiko hayo yalihusu rushwa na yanaendelea kufanyiwa uchunguzi ili kuthibitisha tuhuma na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.
Amesema kuwa malalamiko yasiyohusu rushwa yamepungua kutoka asilimia 54.2 ya robo iliyopita hadi asilimia 23.5, ambapo yameshughulikiwa kwa kutoa elimu, huku baadhi yakielekezwa katika mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Halikadhalika, amesema kuwa upande wa mashtaka, kesi moja imefunguliwa mahakamani, na hivyo kufanya jumla ya kesi tano kuendelea kusikilizwa mahakamani.
Hata hivyo, amesema kuwa TAKUKURU Mkoa wa Temeke imejipanga kuendelea kutekeleza mikakati katika robo ya Aprili hadi Juni 2026, ikiwemo kufuatilia utekelezaji wa maazimio na mapendekezo yaliyotolewa katika vikao kati ya TAKUKURU na wadau.

No comments
Post a Comment