Zinazobamba

BALAMA ALIA NA VITENDO VYA UTEKAJI NA MAUAJI VINAVYOENDELEA

*Amuomba Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia kuingilia kati ili amani iendelee kutawala.

*Ashauri kufungwa CCTV Camera kwenye miji na majiji ili kudhibiti uhalifu haraka.

Na Mussa Augustine.

Mwenyekiti wa Wanawake wa Chama cha NRA Taifa, Bi. Rachel Balama, amemuomba Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwachukulia hatua stahiki za kisheria wale wote wanaobainika kujihusisha na matukio ya mauaji na utekaji.

Mwenyekiti huyo ametoa rai hiyo leo Mei 26, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Vyama 12 rafiki vya siasa kwa lengo la kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kusimama imara katika kuliletea taifa maendeleo.

“Kwa sasa nchi yetu inapitia wakati mgumu sana, hasa katika suala la utekaji na mauaji. Sisi kama wanawake viongozi ndani ya vyama vya siasa tumeona tulizungumzie hili kwa sababu suala la utekaji linaleta hofu kubwa kwa wananchi,” amesema Balama.

Na kuongeza kuwa, “Sisi kama wanawake ndani ya vyama vya siasa tunasikitishwa na tunalaani mawimbi ya matukio ya mauaji na utekaji kwani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 14 na 15, inatambua kuwa kila binadamu ana haki ya kuishi kwa usalama.”

Aidha, amesema kuwa wao kama wanawake viongozi wamemuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu na mtu wa mwisho kuhakikisha masuala ya ulinzi na usalama kwa wananchi yanasimamiwa ipasavyo.

“Tunamuomba Rais aunde tume ya kuchunguza matukio yote ya mauaji na utekaji. Kama kuna watu wanajiteka au wanatekwa, basi tunaomba suala hili aingilie kati kuhakikisha kwamba wale wote wanaofanya vitendo hivyo wanagundulika na wanachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.

Na kuongeza kuwa, “Sisi kama wanawake tunaomba Serikali iimarishe ulinzi wa miji na majiji, aidha kwa kuweka CCTV Camera kwenye maeneo muhimu au kuongeza uwezo wa kiintelijensia wa kiusalama ili kuwatambua wahalifu haraka kabla na baada ya kufanyika kwa matukio ya utekaji.”

Mwenyekiti huyo wa Wanawake wa Chama cha NRA Taifa aidha amesisitiza kuwa amani ya Tanzania ni tunu ya Watanzania wote, hivyo mamlaka za usalama zisiruhusu vikundi vyovyote vya uhalifu kujitokeza kufanya vitendo vinavyowatia hofu wanawake, hususan wakiwa kwenye shughuli zao mbalimbali.

Amesema kuwa wao kama wanawake viongozi ndani ya vyama wana imani na mamlaka ya Rais Dkt. Samia kwa kufanya kazi vizuri na kwamba wasaidizi wake aliowateua wasimuangushe katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, Umoja huo wa Wanawake wa Vyama Rafiki vya Siasa umeundwa na vyama vya NRA, TLP, CCK, DP, SAU, UMD, UDP, NLD, AAFP, ADA TADEA, na MAKINI.

No comments