NONDO KUMPELEKA BABA LEVO MAHAKAMANI

*Ni kutokana na kutoa taarifa za uongo kuwa Nondo alijiteka mara mbili.
*Amtaka amlipe TSh milioni 500 kwa kumdhalilisha, kumkashifu na kutweza utu wake.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mwenyekiti Ngome ya Vijana Taifa Chama Cha Act Wazalendo Abdul Nondo amesema anajiandaa kufungua kesi ya kashfa na udhalilishaji dhidi ya Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, kutokana na kudai kuwa Nondo hakutekwa bali alijiteka.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Mei 23, 2026, Nondo anamshutumu Baba Levo kwa kutoa taarifa za uongo kwa umma ambazo zimemchafua na kumdhalilisha utu wake kuhusiana na matukio mawili ya utekwaji aliyoyapitia.
Aidha, amesema kuwa kupitia wakili wake Hekima Mwasipu wa Matwigwa Law Chambers, ameshatuma barua ya malalamiko Mei 20, 2026 kwa Baba Levo.
Amefafanua kuwa tukio la kwanza la utekwaji wake lilitokea Machi 7, 2018 akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwenyekiti wa TSNP, ambapo alitekwa Dar es Salaam na kutupwa Mafinga mkoani Iringa.
Amesema kutokana na tukio hilo, badala ya kuwa mlalamikaji, aligeuzwa mtuhumiwa na kufunguliwa kesi ya jinai namba 13 ya 2018 kwa kutoa taarifa ya uongo.
Hata hivyo, Novemba 5, 2018, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa chini ya Hakimu Liad Mohamed Chamshama ilimwachia huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo.
Amesema rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka katika Mahakama Kuu Iringa ilitupiliwa mbali Desemba 23, 2019 na Jaji P. M. Kente, aliyesema kuwa DPP ameshindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake.
Pia Mei 11, 2020, DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani, lakini Machi 23, 2022 kabla ya kusikilizwa, DPP aliondoa rufaa hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 77(4), ambapo Nondo anasema alishinda kesi katika ngazi zote tatu za mahakama.
Akizungumzia tukio la pili la utekwaji lililotokea Desemba 1, 2024 saa 11 alfajiri katika Stendi ya Mabasi ya Magufuli, Mbezi Louis, Nondo anadai alitekwa na watu wanne, akapelekwa kwa Land Cruiser nyeupe, akapigwa na kutupwa ufukweni mwa Coco Beach.
Ambapo alisaidiwa na bodaboda hadi ofisi za ACT-Wazalendo Magomeni, kisha kupelekwa Hospitali ya Aga Khan na kulazwa kwa muda wa wiki moja, na kwamba hadi sasa hakuna taarifa ya uchunguzi wa polisi iliyotolewa.
Kufuatia hatua hiyo, Nondo amesema kauli za uongo za Baba Levo zinadhoofisha mapambano dhidi ya matukio ya utekaji yanayoendelea nchini.
Amesema kuwa Baba Levo ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini, ametamka uongo huo mara tatu kupitia chombo chake cha habari cha ‘Seven Media’ Julai 6, 2025, pia kupitia kundi la WhatsApp la Kigoma Yetu Mpya Machi 15, 2026, pamoja na kituo cha televisheni cha Star TV Mei 3, 2026 kwenye kipindi cha Medani Kuu Live kinachoendeshwa na Chief Odemba.
Kufuatia hatua hiyo, Nondo ametoa masharti matatu kwa Baba Levo ndani ya siku saba, ikiwemo kumtaka kuomba radhi hadharani, kuahidi kutoendelea kusambaza uongo, na kumlipa fidia ya shilingi milioni 500. Endapo atashindwa kutekeleza masharti hayo hadi kufikia Mei 30, 2026, atampeleka mahakamani ili athibitishe madai ya kujiteka mara mbili.
No comments
Post a Comment