Tanzania Yasisitiza Umuhimu wa Ushirikiano wa Kikanda katika Nishati ya Nyuklia

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Felchesmi Mramba amesema ushirikiano wa kikanda ni muhimu katika kuharakisha matumizi ya nishati ya nyuklia kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa nishati salama, ya uhakika na yenye kuchochea maendeleo ya uchumi Afrika.
Mha. Mramba ameyasema hayo leo Mei 20, 2026 alipomwakilisha Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi kwenye mjadala wa Mawaziri katika Mkutano wa Pili wa Uvumbuzi wa Nyuklia barani Afrika (NEISA 2026) unaofanyika jijini Kigali, Rwanda.
Akizungumza katika mjadala huo, Mha. Mramba amesema maendeleo ya nishati ya nyuklia hayawezi kufanikiwa kwa kila nchi kufanya kazi kivyake kutokana na gharama kubwa, mahitaji ya miundombinu na utaalamu maalum unaohitajika.
Mha. Mramba ameeleza kuwa Tanzania tayari inawekeza katika miradi ya kuunganisha gridi za umeme na nchi jirani ikiwemo Kenya, Zambia, Uganda, Rwanda na Burundi ili kuboresha usambazaji wa nishati katika ukanda huo.
Aidha Mha. Mramba amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika maendeleo ya wataalamu wa ndani, mifumo madhubuti ya udhibiti pamoja na miundombinu ya kisasa ili kuhakikisha nishati ya nyuklia inachangia ukuaji wa viwanda na uchumi wa muda mrefu.
Mkutano huo wa pili wa uvumbuzi wa nyuklia barani Afrika unafanyika jijini Kigali, Rwanda ambapo ulifunguliwa jana Mei 18, 2026 na Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame ambapo unatarajiwa kuhitimishwa Mei 21, 2026.




No comments
Post a Comment