Zinazobamba

PETROLI YASHUKA, DIZELI YAPATA RUZUKU YA SH. 535


- Tanzania yaendelea kuwa na bei nafuu kulinganisha na nchi nyingi

-Petroli: Tanzania Sh.4,086, Kenya Sh.4,339, Uganda Sh.4,485, Rwanda Sh.5,230, Malawi Sh.9,314 | Dizeli: Tanzania Sh.4,333, Zambia Sh.4,592, Kenya Sh.4,715, Malawi Sh.10,031

Na. Mwandishi wetu,

Licha ya kuendelea kwa mgogoro wa Mashariki ya Kati, kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz na kuongezeka kwa gharama za mafuta katika soko la dunia, Tanzania imeendelea kuhakikisha mafuta yanapatikana nchini huku bei zake zikibaki chini zaidi kuliko nchi kadhaa jirani.

Bei mpya zilizotangazwa na EWURA kuanzia Juni 3, 2026 zinaonyesha kuwa petroli katika Dar es Salaam itauzwa kwa Sh. 4,086 kwa lita, dizeli Sh. 4,333 na mafuta ya taa Sh. 4,685 kwa lita. Aidha, petroli imepungua kwa zaidi ya Shilingi 30 kwa lita ikilinganishwa na mwezi uliopita huku dizeli ikiendelea kubebwa na ruzuku ya Shilingi 534.91 kwa kila lita, sawa na Shilingi 535.

Katika kipindi ambacho mataifa mengi yanakabiliwa na kupanda kwa gharama za nishati na changamoto za upatikanaji wa mafuta, Tanzania imeendelea kuwa na bei nafuu zaidi ya petroli na dizeli miongoni mwa nchi zilizolinganishwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Kwa mujibu wa EWURA, vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta pamoja na kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz ambao hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa duniani, vimeendelea kuongeza gharama za mafuta, usafirishaji na bima za meli katika soko la kimataifa.

Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo, Tanzania imeendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta huku ikidhibiti makali ya bei kupitia hatua mbalimbali ikiwemo ruzuku ya Sh. 535 kwa kila lita ya dizeli.

Hatua hiyo imeendelea kusaidia sekta za usafirishaji, viwanda, kilimo na huduma za kijamii ambazo zinategemea zaidi mafuta hayo.

Wakati dunia ikiendelea kutazama kwa wasiwasi mustakabali wa usambazaji wa mafuta kupitia Hormuz, mwenendo wa mwezi Juni unaonyesha picha tofauti nchini kuwa mafuta yanaendelea kupatikana, petroli imeshuka bei, dizeli imeendelea kupata ruzuku, na Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye mafuta nafuu zaidi katika ukanda licha ya msukosuko mkubwa unaoendelea katika soko la mafuta duniani.

No comments