MWANZA KINARA KATIKA USIMAMIZI WA MAAFA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa Said Mtanda akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Kamati za Usimamizi wa Maafa kwa mkoa wake, yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu leo tarehe 4 Juni, 2026.
Na, mwandishi wetu - Mwanza
Mkoa wa Mwanza umetajwa kuwa Kinara kwa kuratibu na kusimamia ipasavyo shughuli za kukabiliana na maafa, majanga na mawasiliano ya dharura kutokana na hatua mbalimbali za kuimarisha mifumo ya utayari na mwitikio wa dharura.
Sifa hizo zimetolewa Juni 4, 2026 na wataalamu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa mafunzo ya Kamati za Usimamizi wa Maafa yanayofanyika mkoani Mwanza kwa siku mbili yakilenga kuongeza uwezo wa kukabiliana na majanga.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa Said Mtanda amesema maafa yameendelea kuwa tishio kubwa duniani kutokana na athari zake kwa maisha ya watu, uchumi na maendeleo ya jamii.
Ametaja baadhi ya majanga yanayoikabili Tanzania kuwa ni mafuriko, ukame, maporomoko ya ardhi, matetemeko ya ardhi, mioto ya misitu na magonjwa ya mlipuko.
Kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo Mhe. Mtanda amezitaka Wilaya zote Mkoani humo kuwa na mipango kazi na mifumo imara ya usimamizi wa maafa ili kuhakikisha maandalizi, mwitikio wa haraka na urejeshaji wa hali unafanyika kwa ufanisi.
Aliongezea kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuimarisha usimamizi wa maafa kwa kutumia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2024 pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo viongozi na wataalamu katika utekelezaji wa sera, sheria na miongozo ya usimamizi wa maafa katika maeneo yao.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa msaada kwa waathirika wa mafuriko Wilayani Kwimba, uliojumuisha tani tisa za mahindi, mablanketi, ndoo na vifaa vya wanafunzi.
Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Usimamizi wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Bi. Wilfrida Ngowi akiwasilisha mada kuhusu Dhana ya Usimamizi wa Maafa wakati wa mafunzo ya Kamati za Usimamizi wa Maafa mkoa wa Mwanza, yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.Mafunzo yamefanyika tarehe 4 Juni, 2026.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Maafa eneo la utafiti kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bw. Vanvaco Luvanda amesema mafunzo hayo ya siku mbili yanaendelea kutolewa nchini kote kwa lengo la kuongeza utayari na uwezo wa kitaalamu wa kukabiliana na maafa yanapotokea.
Alifafanua kuwa, uwepo wa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka ambapo uzoefu unaonesha kuwa athari za maafa zinaendelea kuongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la shughuli za kibinadamu na changamoto nyingine zinazoweza kusababisha maafa.
Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Usimamizi wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Bi. Numpe Mwambenja akiwasilisha mada kuhusu Nyenzo za Usimamizi wa Maafa wakati wa mafunzo ya Kamati za Usimamizi wa Maafa kwa mkoa wa Mwanza.Mafunzo yamefanyika tarehe 4 Juni, 2026.
Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Usimamizi wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Bi. Dorothy Pantaleo akiwasilisha mada kuhusu Mfumo wa Usimamizi wa Maafa wakati wa mafunzo ya Kamati za Usimamizi wa Maafa kwa mkoa wa Mwanza.Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.


Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa kwa mkoa wa Mwanza, wakifuatilia mada zilizowasilishwa wakati wa mafunzo ya Kamati hizo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu tarehe 4 Juni, 2026
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
No comments
Post a Comment