Zinazobamba

TMA Yatahadharisha Jamii Athari za Kipupwe


Na Mussa Augustine

Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) imeishauri jamii kuchukua hatua stahiki za kiafya ili kujikinga na magonjwa yanayoweza kusababishwa na hali ya hewa ya baridi na vumbi.

Ushauri huo umetolewa leo Mei 25, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang'a, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mwelekeo wa hali ya kipupwe katika kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti (JJA) mwaka huu.

Dkt. Chang'a pia amewashauri wafugaji kuendelea kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo ili kudhibiti visumbufu na magonjwa pamoja na kufuata ushauri wa wataalamu, na maji na malisho yanapaswa kutumika kwa uangalifu ili kupunguza athari zinazotarajiwa.

Halikadhalika, amewashauri wakulima kulima kwa kuzingatia ushauri wa maafisa ugani katika maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua katika kipindi hiki cha msimu wa kipupwe.

"Kwa watumiaji wa bahari, taarifa hii itasaidia kupunguza athari za upepo unaotarajiwa. Pia, sekta za ujenzi, madini na uchukuzi zinatarajiwa kunufaika kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa," amesema.Aidha, ameendelea kusema kuwa taarifa hiyo watumiaji wengine wote waitumie ipasavyo na wanashauriwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa zikiwemo utabiri wa kila siku, angalizo na tahadhari ili kuongeza ufanisi na usalama wa shughuli zao.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chang'a amesema kuwa kwa kawaida msimu wa kipupwe hutawaliwa na upepo wa kusini ambapo msimu wa kipupwe 2026 unatarajiwa kutawaliwa na upepo uliopungua nguvu kidogo kama ilivyo kawaida, utakaovuma kutoka kusini mashariki kwa maeneo mengi ya nchi, na vipindi vichache vya upepo mkali utakaovuma kutoka kusini hususan katika kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2026 katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.

Aidha, amesema kuwa kwa kawaida kipindi cha msimu wa kipupwe (JJA) hutawaliwa na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi, ambapo kwa JJA 2026, vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria hususan Mkoa wa Mara pamoja na ukanda wa pwani na maeneo ya nchi kavu (mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi na Pwani ikijumuisha Kisiwa cha Mafia pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) na sehemu zenye miinuko za nyanda za juu kaskazini mashariki.Aidha, amesema kuwa katika kipindi cha msimu wa Juni hadi Agosti 2026, joto la bahari katika ukanda wa tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuwa juu ya wastani, hali inayoashiria kujijenga kwa hali ya El Niño.

Amesema kuwa kwa Bahari ya Hindi, joto la juu ya wastani linatarajiwa katika maeneo ya magharibi mwa bahari hiyo (pwani ya Afrika Mashariki) na joto la wastani linatarajiwa katika maeneo ya mashariki (pwani ya Indonesia).

Vilevile, upepo wa bahari wenye unyevunyevu uvumao kutoka mashariki unatarajiwa kuelekea katika maeneo ya ukanda wa pwani. Hali hii inatarajiwa kuongeza msukumo wa unyevunyevu kutoka baharini kuelekea nchini pamoja na kupunguza baridi ya wakati wa usiku kwa kuongeza kiwango cha chini cha joto na kusababisha mvua za nje ya msimu.Kwa upande mwingine, joto la bahari katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi (kusini mwa Kisiwa cha Madagascar) linatarajiwa kuwa juu ya wastani. Hali hii inatarajiwa kudhoofisha mgandamizo mkubwa wa hewa katika eneo hilo na hivyo kupunguza kasi ya upepo wenye baridi kutoka kusini kuelekea katika maeneo ya nchi yetu.



No comments