DOYO AMPONGEZA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KWA KUVICHUKULIA HATUA CCM NA CHADEMA

*NLD Yapongeza Msajili, Doyo Ataka Uwajibikaji wa Kisiasa kwa Vyama Vyote Bila Ubaguzi
Na Mwandishi wetu:TANGA
Chama cha National League for Democracy (NLD) kimesema hatua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuvitaka vyama vya CCM na CHADEMA kutoa maelezo kuhusu kauli za baadhi ya viongozi wao ni ishara ya usimamizi wa haki na usawa kwa vyama vyote vya siasa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga leo, Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo, alisema uamuzi huo unaonyesha kuwa sheria na taratibu za kisiasa zinaweza kutekelezwa kwa usawa bila kuangalia ukubwa au nguvu ya chama husika.
Doyo alieleza kuwa hatua ya Msajili kuviandikia barua vyama hivyo viwili imeondoa hisia za upendeleo ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara katika utekelezaji wa sheria zinazohusu vyama vya siasa.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa sheria kwa usawa unasaidia kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi zinazosimamia mfumo wa kisiasa pamoja na kudumisha misingi ya haki, uwajibikaji na utawala wa sheria.
Pamoja na hayo, NLD limewataka viongozi wa kisiasa pamoja na wanachama wa vyama mbalimbali kuwa waangalifu katika matamshi yao na kuzingatia sheria pamoja na taratibu za nchi ili kulinda amani, mshikamano na utulivu wa taifa.
Hivi karibuni, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilivitaka CCM na CHADEMA kuwasilisha maelezo kufuatia matamshi yaliyotolewa na baadhi ya viongozi na makada wa vyama hivyo.
No comments
Post a Comment