WACHIMBAJI MADINI WAITWA CHUNYA KUPATA ELIMU YA UCHIMBAJI UNAOZINGATIA UHIFADHI WA MAZINGIRA.
Kampeni ya uchimbaji wa Madini unaozingatia kulinda Mazingira "Green Mining Awareness"inayoendeshwa na taasisi ya TWC,ina mpango wa kuwakutanisha wadau wa sekta ya madini nchini kujadili changamoto zinazowakabili na kupata elimu ya uchimbaji unaozingatia uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari April 2,2026 jijini Dar es salaam Mratibu wa kampeni hiyo John Paul Salita amebainisha kwamba wadau hao watakutana Aprili 17 mwaka huu, Wilayani Chunya Mkoani Mbeya ili kuwasaidia kupata elimu ya matumizi ya teknolojia salama.
"Siku hiyo tutawaeleza umuhimu wa kutumia teknolojia salama,kufuata sheria, kuwa na leseni pamoja na kuepuka kutumia mbinu zisizo salama ikiwemo za kishirikina katika uchimbaji madini," amesema Salita
Nakuongeza kuwa "tunamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Madini chini ya Waziri Anthony Mavunde kwa kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya Madini,hivyo na sisi kama wadau hatuna budi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya Madini nchini,".
Aidha ameongeza kuwa taasisi za kibenki ikiwemo NMB,kampuni zinazouza na kukopesha vifaa vya uchimbaji madini ikiwemo kampuni ya RM Kyando,Kaeser Compressor na nyinginezo zitakuwepo kwenye mkutano huo ili wachimbaji waweze kuelewa njia sahihi za kuweza kununua au kukopeshwa ili wafanye shughuli za uchimbaji nakufikia malengo yao.
Kwa upande wake Balozi wa kampeni ya Green Mining Awareness Anna Nyange amesema kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa kuendeleza mabadiliko makubwa katika kuijenga Sekta ya Madini iliyoendelevu na yenye manufaa kwa wachimbaji wote pamoja na Taifa kwa ujumla.
"Ninawaomba wadau wajitokeza kwa wingi katika mkutano huo wenye fursa zote za elimu,teknolojia na mitandao ya kibiashara ambapo wachimbaji watakutanishwa na wafanyabishara mbalimbali wa teknolojia za kisasa pamoja taasisi za kifedha ili kupata njia sahihi ya kufanikiwa kwenye shughuli zao"amesema Nyange.





No comments
Post a Comment