WANANCHI WAPATAO 2000 WAMEJISAJILI KUPATA KITAMBULISHO CHA TAIFA KATA YA BUYUNI.
Baadhi ya Wananchi wa kata ya Buyuni wakisubiri huduma ya kujisajili kupata kitambulisho cha Taifa (NIDA).Na Mussa Augustine.
Zaidi ya Wananchi 2000 wamesajiliwa kwa ajili ya kupata kitambulisho cha Taifa (NIDA) katika kata ya Buyuni Halmashauri ya Jiji la Dar,ambapo zoezi hilo liliratibiwa kupitia Ofisi ya Diwani wa Kata hiyo pamoja na Mamkala ya Vitambulisho vya Taifa NIDA.
zoezi hilo limeanza rasmi Januari 19,2026 na limehitimishwa jana Januari 30,2026 katika kata ya Buyuni huku Wananchi wakiomba kuongeza siku ili wale ambao bado hawajafanikiwa kujisajili kutokana na sababu mbalimbali waweze kunufaika na fursa hiyo.
Baadhi ya Wananchi hao akiwemo Jamaldin Amri,Salama Kumbi,Rehema Jabiri Kabri,na Andrew William Bundala wamezungumza kwa nyakati tofauti nakubainisha kuwa changamoto kubwa iliyowakumba Wananchi wengi ni kukosa kitambulisho cha kuzaliwa hali ambayo imewafanya wengi wao washindwe kujisajili.
Jamalidin Amri amesema zoezi hilo limekwenda vizuri na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na usimamizi mzuri wa viongozi wa kata pamoja na ushirikiano kutoka Serikalini.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea zoezi hili katika kata yetu,uandikishaji umeenda vizuri na tunawashukuru viongozi wetu kwa kutusimamia ipasavyo,hata hivyo,bado kuna wananchi wengi wanaohitaji huduma hii, hivyo tunaomba zoezi liwe endelevu,” amesema Jamaldin.
Nakuongeza kuwa"mahitaji ya vitambulisho vya Taifa ni makubwa kwa wananchi,hivyo kuendelezwa kwa zoezi hilo kutasaidia kupunguza changamoto kwa wananchi wanaokosa huduma mbalimbali zinazohitaji kitambulisho cha Taifa(NIDA).
Nae Salama Kumbi mkazi wa kata hiyo ya Buyuni,amesema kampeni hiyo ya kutoa vitambulisho vya Taifa imefanikiwa na kuwasaidia wananchi waliokuwa na changamoto kwa muda mrefu kupata huduma hiyo,nakwamba watakaopata vitambulisho hivyo wataweza kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake,Vijana na watu wenye ulemavu.
“Zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya NIDA limeenda vizuri,hapo awali nilikuwa na changamoto,lakini leo hii nimemaliza zoezi langu,tunawashukuru viongozi wetu hususani Diwani wa Kata hii ya Buyuni Mheshimiwa Jesica Msolla kwa jitihada zake za kutuletea huduma hii karibu yetu,” amesema Salama.
Vilevile Rehema Jabir amesema changamoto kubwa katika utekelezaji wa zoezi hilo ilikuwa ni wingi wa wananchi pamoja na foleni ndefu,hata hivyo wananchi wengi wamefanikiwa kupata huduma hiyo kwa ufasaha mkubwa.
“Tunashukuru uongozi wetu wa kata kupitia Diwani Jesica Msolla,ambaye ametupambania wananchi wake kwa kuondoa usumbufu wa kufuata huduma za NIDA maeneo ya mbali,” amesema Rehema.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo, Jesica Mahamoud Msolla amesema kuwa zoezi hilo limemalizika vizuri huku zaidi ya wananchi 2000 wamejitokeza kujisajili kupata huduma hiyo.
Diwani wa Kata ya Buyuni Jesica Mahmoud Msolla.Amesema zoezi hilo limeweza kufikia Wananchi wa mitaa nane ya kata hiyo,nakwamba zoezi hilo limekwenda vizuri kwani watu wengi wamepata huduma hiyo.
"Tumeweza kuwafikia watu wengi lakini bado kuna uhitaji wa huduma hii kwa wananchi,hivyo tumeomba mamlaka husika ziweze kuona umuhimimu wa zoezi hili ili liweze kuongzewa muda na liwe endelevu" amesema Mh.Msolla
Aidha amewaasa wananchi wa kata hiyo kufuata maelezo yote yanayotolewa na Serikali ya kata hiyo na kuepuka madalali au vishoka ambao wanawadaganya kutoa fedha ili wapate kitambulisho cha Taifa.
Halikadhalika kaimu Mtendaji wa Kata ya Buyuni Prisca Mwaijande amesema kuwa zoezi hilo limefanyika kwa ustadi mkubwa kutokana na mwitikio wa wakazi wengi waliofika kujisajili kupata NiDA.
Nae Mwenyekiti wa Mtaa wa Buyuni Sylvanus Mwenda amesema kwamba wanajaribu kuongea na mamlaka zinazohusika ikiwemo NIDA na Uhamiaji,ili walifanye zoezi hilo kua endelevu.
Ikumbukwe kuwa zoezi la usajili wa Wananchi kupata kitambulisho cha NIDA katika Jimbo la Ukonga limefanyika kuanzia Januari 19,2026 katika kata za Buyuni na Chanika, ambapo Wananchi wataanza kupata vitambulisho hivyo baada ya siku 21 kuanzia Februari 1,2026.



.jpg)


No comments
Post a Comment