Zinazobamba

JESHI LA POLISI KANDA MAALUMU YA DAR ES SALAAM LINAENDELEA KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA WA RAIA: KAMANDA MULIRO


Na Mwandishi Wetu.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria pamoja na wananchi, limeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha hali ya usalama katika maeneo tofauti ya jiji.

Hayo amebainishwa na Kamanda wa kanda hiyo Jumanne Muliro wakati akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Januari 31,2026 ambapo amesema kiipaumbele cha Jeshi hilo ni kusimamia mifumo madhubuti ya kuzuia na kudhibiti vitendo vya kihalifu ili kulinda usalama wa raia na mali zao.

"Makosa dhidi ya binadamu yameendelea kuwa chukizo kubwa kwa jamii, yakiwemo mauaji, ubakaji, ulawiti, kutorosha wanafunzi pamoja na kuwapa mimba wanafunzi,kupitia ofisi za Mashtaka na Mahakama,Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wa makosa hayo" amesema Kamanda Muliro 

Aidha amesema kuwa kati ya mwezi Desemba 2025 na Januari 2026, baadhi ya kesi zilizofikishwa mahakamani na kufikia hatua ya mwisho ziliwezesha watuhumiwa kupatikana na hatia na kuwataja kuwa Miongoni ni Peter Julius, mkazi wa Mbezi Mwisho, aliyefungwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo kwa kosa la ulawiti.

Mwingine ni Dunia Sadick (Dunia),mkazi wa Chanika, aliyefungwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa kosa la kubaka.

Pia Rajab Rashid Goma,mkazi wa Mwanagati, aliyefungwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa kosa la ulawiti.

Huku John Jacob Nyamahemba, mkazi wa Mbagala,aliyefungwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa kosa la kubaka.

Na Abdallah Faustin,mkazi wa Kibada, aliyefungwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni kwa kosa la kubaka.

Pamoja na Abubakar Jumanne Membe (Abuu), mkazi wa Mbagala, aliyefungwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa kosa la ulawiti.

Akizungumzia kuhusu suala la usalama barabarani Kamanda Muliro amesema, jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani limeendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara,nakutoa onyo kali kwa madereva wa vyombo vya moto wanaokiuka sheria za usalama barabarani. 

"Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya madereva wazembe, wakiwemo wanaopita kwenye barabara za mabasi ya mwendokasi kinyume cha sheria." Amesema Kamanda Muliro 

Katika hatua nyingine Kamanda Muliro amesema jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es salaam linatambua kuwepo kwa mchezo wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa klabu ya Simba dhidi ya Esparance de Tunis utakaofanyika siku ya Jumapili Februari 01,2026 majira ya saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam,hivyo jeshi hilo limewahakikishia wapenzi na mashabiki wa soka kuwepo kwa usalama wa kutosha ndani na nje ya uwanja hivyo.

No comments