Zinazobamba

UJENZI WA BARABARA YA ZAVARA KATA YA BUYUNI WAIVA.


Na Mussa Augustine.

Diwani wa kata ya Buyuni Jesica Mahmoud Msolla ameambatana na maafisa kutok Wakala wa Barabara Mijini na  Vijijini (TARURA)Halmashauri ya Jijini la Dar es salaam kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Zavara yenye urefu wa Kilometa 4 pamoja na kivuko cha Kidongo chekundu,ambapo ujenzi huo unaanza mapema mwezi februari mwaka huu.

Akizungumza jana Januari 30,2026 na Waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo Diwani huyo amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo utafanywa na kampuni ya Bronze  Tech.Co.Ltd ambayo imepewa zabuni hiyo na Serikali.

"Leo(jana)tumetembelewa na maafisa kutoka TARURA kwa ajili ya kuangalia miradi yetu ya barabara,nilishaanza kufuatilia vivuko hatarishi kwa wakazi wa kata yangu ya Buyuni katika mitaa yote nane,kwa leo tumeanza na mradi ambao upo mtaa wa Zavara ambako kuna kivuko kinajengwa kwa kiwango cha juu kitaalamu,ujenzi huo utawezesha Wananchi wa mitaa ya Kigezi, Buyuni,Zavara na jirani zetu wa kata ya Kivule kupitia Majohe wataweza kupita kwa urahisi maana barabara ile ina urefu wa Kilometa 4."amesema Mh.Msolla.
Nakuongeza"Namshukuru sana Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fungu hilo,bajeti ipo tayari na mkandarasi Bronze Tech ndio waliokabidhiwa zabuni hiyo na Serikali, hivyo tarehe 10 mwezi wa pili nawaalika wakazi wote wa kata ya Buyuni waje washuhudie mitambo itakua eneo la mradi na ujenzi utaanza rasmi,naomba Wananchi watoe ushirikiano ."

Kwa upande wake Afisa kutoka TARURA Halmashauri ya Jiji la Ilala Eng.Fadhili Sadara amesema ujenzi wa miradi hiyo utakua wa maeneo mawili ambapo eneo la kwanza ni mradi wa Zavara,huku mradi wa pili utaanza hapo baadae baada ya kukamilika kwa mchanganuo ambao ni mradi wa barabara ya Mgeule.

"Eneo la kwanza ni pale Zavara ambapo tayari mradi umeshaanza na mkandarasi yupo eneo la mradi(site),ambapo utahusisha ujenzi wa kivuko "Boksi Karavati" na barabara isiyopungua Kilometa 4,tumetembelea eneo lote la mradi na mkandarasi yupo tayari kuanza kutekeleza ujenzi huo,eneo la pili ni hapa Mgeule tumeona kuna daraja la miti,tumeshauriana na mheshimiwa Diwani kwamba tujenge daraja la aina ya Boksi Karavati kama ilivyo kule Zavara." 

Nakuongeza"tumemuahidi mheshimiwa Diwani tutarudi wakati mwingine ili tufanye tathmini ili kuweza kuandaa michoro pamoja na mchanganuo wa ujenzi wa Karavati hiyo,baada ya hapo utafuata utekelezaji ambao utahusisha ujenzi wa daraja lenyewe pamoja na barabara ya Mgeule kwani tunaona pia inachangamoto,na gharama za mradi huu zitajulikana baada ya kufanya mchanganuo".

Awali Mwenyekiti wa Mtaa wa Zavara Faridu Rashidi Sadiki amesema kuwa kukamilika kwa daraja la Kidongo chekundu utasaidia kuondoa adha wanayoipata Wananchi wa Mtaa huo pamoja na mitaa mingine ya Kata ya Buyuni na kata jirani.

"Huu mradi ukikamilika utasaidia sana wakazi wa Zavara na mitaa mingine jirani ambao kwa sasa wanapata tabu sana kutoka kwenye barabara kuu ya lami kuja huku mtaani hususani kipindi cha mvua kwani inabidi wapite kwenye kata zingine ndo waje huku kata ya  Buyuni" amesema.Sadiki.

Nae mwakilishi wa Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mgeule,Bi.Marry Kiango amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Mgeule pamoja na barabara utasaidia kuondoa changamoto ambayo Wananchi wa Mtaa wa Mgeule wamekua wakiipata kwa muda mrefu.
   Daraja la Mgeule likionekana likiwa         limetengezwa kwa miti,hali ambayo Wananchi wanapata usumbufu mkubwa wakati wa kuvuka.

"Namuomba sana Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan aweze kuridhia kutoa fedha kwa ajili ya kujenga daraja hili la Mgeule ambalo kwa sasa tumewekewa daraja la miti ambalo sio salama kwa wakazi wa mtaa huu na mitaa mingine wanaopita kwenye daraja hilo. 

Hata hivyo mwakilishi wa Kampuni ya Bronze Tech.Co.Ltd ,Athuman Kimomwe amemhakikishia Diwani Msolla na maafisa wa TARURA kuwa ujenzi wa barabara ya Zavara na kivuko hicho utakamilika kwa muda uliopangwa kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba.








No comments