TEITI yashiriki Maonesho ya 8 ya Uwekezaji katika Sekta ya Madini Mkoani Geita
*Tanzania yaendelea kutekeleza kwa ukamilifu Vigezo vya Kimataifa vya EITI
*Uwazi wa Mikataba katika sekta ya uziduaji waanza kutekelezwa.
Na Mwandishi Wetu.Geita.
Taasisi ya Uangalizi wa Rasilimali za Uziduaji Tanzania (TEITI) imeshiriki katika Maonesho ya 8 ya Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayofanyika Mkoani Geita, yaliyofunguliwa rasmi Septemba 22, 2025 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Akizungumza Septemba 23, 2025, Meneja wa Kitengo cha Uwazi na Uwajibikaji kutoka TEITI, Bw. Erick Ketagory, alisema tangu Tanzania ijiunge na Asasi ya Kimataifa ya EITI yenye makao yake makuu nchini Norway, imeendelea kutekeleza kikamilifu vigezo vya Kimataifa vya EITI vya mwaka 2023 sambamba na Sheria ya TEITA ya mwaka 2015.
Aliongeza kuwa, katika tathmini ya hivi karibuni iliyofanywa na Umoja wa EITI, Tanzania imepata matokeo chanya kwa kuonyesha utekelezaji kamili wa vigezo hivyo.
Bw. Ketagory alibainisha kuwa, kati ya mwaka 2009 hadi 2025, TEITI imetoa jumla ya ripoti 15 za ulinganishi wa malipo ya Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia na mapato ya Serikali. Aidha, ripoti ya 15 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ilitolewa rasmi Juni 30, 2025Kwa upande mwingine, Bw. Ketagory alisisitiza kuwa TEITI imeanza kutekeleza sharti la uwazi wa mikataba, ambapo mikataba ambayo Serikali imeingia na kampuni za sekta ya uziduaji sasa imewekwa wazi kupitia tovuti ya TEITI.
“Tunawaalika wananchi wote wa Mkoa wa Geita kutembelea banda la TEITI ili kujifunza zaidi kuhusu majukumu ya TEITI pamoja na namna ya kutumia takwimu zinazotolewa kupitia ripoti zake,” alihitimisha Bw. Ketagory.
Taarifa na ripoti zote za TEITI zinapatikana kupitia tovuti: www.teiti.go.tz
No comments
Post a Comment