Zinazobamba

TANESCO YATOA WITO KWA WANANCHI KUHAKIKI MITA KABLA YA KUNUNUA AU KUPANGA JENGO


📌Yasema ni hatua muhimu ya kuwaepusha na adhabu za kisheria 

📌Wito huo ni kufuatia kukithiri kwa matukio ya uhamishaji wa mita kinyume cha utaratibu 

Na Agnes Njaala, Temeke Dar es Salaam

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa wito kwa wateja na wananchi kwa ujumla kuhakikisha taarifa za mita za umeme zinahakikiwa kabla ya kununua au kupanga jengo ikiwa ni hatua muhimu ya kuwaepusha na matumizi yasiyo halali ya umeme yatakayopelekea usumbufu wa kusitishiwa huduma ikiambatana na adhabu za kisheria.Akizungumza, katika zoezi la ukaguzi wa mita linaloendelea Kanda ya Mashariki, Fundi Sanifu Kitengo  cha Udhibiti Mapato TANESCO Kanda ya Mashariki Bw. Yasin Bakari alisema kuwa ukaguzi  uliofanyika  Septemba 20, 2025 katika baadhi ya maeneo Mkoa wa Temeke umebaini baadhi ya mita kuhamishwa kinyume na taratibu na nyingine kuchepushwa nyaya ili kuruhusu matumizi ya umeme bila kuhesabiwa kwenye mita. 

Ametaja idadi ya mita zilizobainika kuhamishwa ni tatu (3) ikiwemo mita aina ya Inhemeter iliyohamishwa kutoka Ilala kwenda Tandika Shule, Bahdela iliyohamishwa kutoka Mtoni Mtongani kwenda Ugweno Tandika, na EDMI iliyohamishwa kutoka Kurasini Bwawani kwenda Likwati Temeke na wakati huo huo mita mbili aina ya Wasion na Actaris katika maeneo hayo hayo zimebainika pia kuchepushwa nyaya na kuwezesha wizi wa umeme. Aliongeza kuwa, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kung’oa mita hizo, ambapo wahusika watapaswa kulipa faini na kuwasilisha maombi mapya ya huduma ya umeme huku waliochepusha nyaya, watalazimika kulipa deni lote la matumizi yaliyofanyika kinyume cha taratibu.

Aidha , uchunguzi umethibitisha kuwa baadhi ya wateja wanafanya vitendo hivyo wakikwepa  gharama za kufuata utaratibu halali wa kuomba huduma mpya ya umeme wanapohama makazi jambo linalosababisha hasara kwa shirika na kuathiri ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma bora na endelevu. Shirika linatoa rai kwa wateja wote kushirikiana kwa kuhakikisha wanazingatia taratibu sahihi za kupata huduma ya umeme kwa usalama wao. Kufanya hivyo kutasaidia kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, inayowezeshwa na pato la Taifa.



No comments