Zinazobamba

Doyo Azuru Butiama, Aahidi Kuenzi Mchango wa Baba wa Taifa.

*Asisitiza Amani, Umoja na Mshikamano, Kupiga Vita Ukabila na Udini”

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Doyo Hassan Doyo, amefanya ziara maalum katika kijiji cha Butiama, mkoani Mara, ambapo alizuru kaburi la Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Akiwa Butiama, Mhe. Doyo aliweka msisitizo mkubwa katika kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, akibainisha kuwa fikra na maono ya Mwalimu Nyerere ndiyo msingi wa kudumisha amani ya nchi, mshikamano wa kitaifa, na kupiga vita vitendo vya ukabila na udini. Alisema kuwa taifa litaendelea kuwa imara iwapo Watanzania wote wataendeleza misingi ya umoja, upendo, na mshikamano aliouacha Mwalimu.

Mhe. Doyo pia alifafanua kuwa sera ya Uzalendo, Haki na Maendeleo ya chama chake cha NLD imetokana moja kwa moja na fikra na falsafa za Mwalimu Nyerere. Alisisitiza kuwa ndiyo maana Ilani ya Uchaguzi ya NLD imebeba tunu za uzalendo, haki, na maendeleo, kwa lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere na kuendeleza urithi wake wa kisiasa na kijamii.

Katika hotuba yake, alisisitiza dhamira yake ya kupunguza maslahi ya wabunge iwapo atachaguliwa kuwa Rais, akieleza kuwa hatua hiyo ni kielelezo cha dhati cha kumuunga mkono Mwalimu Nyerere, ambaye alipigania siasa safi, usawa, na uwajibikaji kwa viongozi wa umma.

Mhe. Doyo alihitimisha kwa kuwataka Watanzania kuungana pamoja bila kujali tofauti zao za kidini, kikabila au kisiasa, akisisitiza kuwa amani, mshikamano, na uzalendo ndio nguzo kuu za maendeleo ya taifa, huku akiwataka Watanzania kuwa wazalendo kwa Taifa lao.

Msafara wa mgombea urais huyo wa NLD upo mkoani Mara, na kesho kampeni za chama hicho zitaendelea katika Wilaya ya Bunda.

No comments