MWIRU AWAHAKIKISHIA SOKO LA UHAKIKA LA KOROSHO,MBAAZI NA UFUTA WANANCHI WA TANDAHIMBA.
Mgombea urais wa Chama Cha Wakulima (AAFP)Kunje Ngombale Mwiru amewambia Wananchi Wilayani Tandahimba kuwa endapo watamchagua Oktoba 29 mwaka huu kua rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,ataongeza bei ya mazao ya Korosho,Mbaazi na Ufuta.
Amesema hayo leo Septemba 23,2025 katika Viwanja vya forodhani Wilayani Tandahimba Mkoani Mtwara wakati akinadi Ilani ya chama hicho nakuwaomba wananchi kukipigia kura za ndio kwenye uchaguzi mkuu ili kiweze kuwaletea maendeleo ya lazima naya kweli.
Mheshimiwa Mwiru amesema kuwa akishika madaraka atahakikisha zao la ufuta limepanda bei,na zao la Mbaazi litauzwa kiasi cha shilingi elfu tano(5,000)kwa kilo,huku Korosho itauzwa shilingi elfu kumi(10,000)kwa kilo.
Aidha amesema kuwa atajenga masoko maalumu ya kuuza mazao yote yanayotoka kanda ya kusini,ambapo pia anampango Mkoa wa Lindi au Mtwara kujenga soko kuu la kanda kwa ajili ya kuuza mazao hayo.
"Tena kutakuwa na mtaa,sio naweka vijumba vidogovidogo kwa ajili ya kununua ufuta nyie Wakulima ni matajiri,nitajenga nakuandika kabisa mtaa huu ni mtaa wa ufuta,najenga eneo jingine naandika kabisa huu ni mtaa wa korosho,yaani nitachukua eneo kubwa mkulima ukienda kuuza mazao yako hautahangaika"amesema.
Nakuongeza kwamba "Wanatandahimba kwenye masuala ya kilimo labda mniangushe nyie,leo tuna chama chetu cha wakulima(AAFP),hichi ndio chama chenu,leo ukija hapa Tandahimba unaweza kukutana na vyama zaidi ya vitano vya ushirika,halafu wao wanaota vitambi tu mkulima wangu anapata shida,
tarehe 29 mwaka huu mkinichagua vyama hivyo sijui AMCOS sijui nini, stakabadhi ghalani navifutilia mbali,nichagueni muone mabadiliko ya lazima naya kweli.
"Amesema kuwa Viongozi wa serikali wakienda sheli hawakopi mafuta,lakini wakulima wanalima mwaka mzima mazao yao,lakini wanapovuna wanambiwa kuuza kwa mfumo wa stakabadhi ghalani hali ambayo sio sawa ni kumdidimiza mkulima kimaendeleo.
"Wanaoleta mifumo hii ni madalalidalali tu wanajenga vijumba vyao huko matumbo mbelembele tu,hapa sasa nitawapeleka kwenye bwawa la mamba tarehe 29 mwaka huu mkinichagua kua rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mgombea mwenza wangu Chum Abdalah Juma"amesema
Aidha mheshimiwa Mwiru ameendelea kufafanua kwamba mafisadi hawapo ngazi za juu pekee bali wanajifunza kuanzia ngazi za chini hadi wanakua mafisadi sugu,serikali yake hatakua na huruma nao bali atahakikisha linajengwa bwawa la mamba Ikulu kwa ajili ya kuwaadhibu.
"Mara amekua dalali wa korosho, wa ufuta,wa karanga,wa mbaazi,hata hizo bei mnazoletewa huo ni mpango tu watu wanataka kuwaburuzeni tu,ndo maana bei ya mbaazi imeshuka kwa sasa mnauza shilingi mia tatu(300) kwa kilo,najiuliza kwani imekua biskuti,kwakweli hawana huruma hawa watu."amesema.
Hata hivyo Mgombea huyo wa urais kupitia Chama Cha Wakulima AAFP,ameendelea kutoa ahadi zake za kuboresha katika sekta mbalimbali ikiwemo Elimu,Afya na Barabara.
*Kuhusu Elimu.
Amesema kuwa atahakikisha walimu wanajengewa nyumba bora pamoja na kulipwa mshahara mnono kwani wanafanya kazi kubwa ya kufundisha maprofesa ambapo wengine ndio wanakua mafisadi wakubwa.
*Jeshi la Polisi.
Ameendelea kusisitisza kuwa askari polisi wataboreshewa maslahi yao,ikiwemo kupewa nyongeza za mshahara kwani wamekua wakifanya kazi kubwa ya kulinda Wananchi na mali zao.
*Sekta ya Afya.
Amewambia wananchi wa Tandahimba kuwa Serikali yake itajenga nyumba za watumishi katika eneo la vituo vya Afya ili wanapopatwa na ugonjwa wa ghafla iwe rahisi kupata matibabu, nakwamba kutakua na miundominu yote muhimu ikiwemo maji na umeme.
*Miundombinu ya Barabara.
Ataweka mashine ya kuponda mawe(Crusher)kila Wilaya ili kuhakikisha barabara zote zinajengwa kwa kiwango cha zege kwani Tanzania ina rasilimali milima,pamoja na kuwepo kwa Viwanda vingi vya saruji(Cement )na nondo,hali ambayo pia itasaidia kutoa ajira kwa Vijana kwa kushiriki kwenye miradi ya ujenzi wa barabara hizo.

*Kuwezesha Vijana kiuchumi.
Amesema kuwa Serikali yake itahakikisha kila kijana alietimiza umri wa miaka 18 atapatiwa pikipiki bure kwa ajili ya kumuinua kiuchumi.
*Kila kaya 10 zitapatiwa trekta ya Kilimo.
Amesema kuwa Serikali yake itatoa trekta moja kwa kila kaya 10 kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo na kujiinua kiuchumi.
*Michezo na burudani.
Aidha amesema kwamba atahakikisha Wilaya ya Tandahimba inakua na uwanja wa mpira wa kisasa pamoja na kuwepo kwa timu bora itakayoleta ushindani mkubwa,hali ambayo itasaidia kuinua vipaji vya soka kwa Vijana.
No comments
Post a Comment