HIFADHI YA MPANGA-KIPENGERE YAKONGA NYOYO ZA WALIMBWENDE MISS UNIVERSE 2025
📍Rais Samia Apongezwa uboreshaji Miundombinu
Na Beatus Maganja, Mbeya
Walimbwende wa Miss Universe Tanzania 2025 wametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na maono yake ya kukuza sekta ya utalii nchini kupitia maboresho ya miundombinu ya Hifadhi ya Mpanga Kipengere jambo linaloifanya Hifadhi hiyo kuwa kivutio kikubwa cha watalii nyanda za juu kusini.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 29, 2025 na walimbwende hao mara baada ya kufanya ziara maalum katika hifadhi hiyo iliyopo Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA ambapo walibaini fursa kubwa ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia urithi wa asili wa eneo hilo."Tumeona historia ya Chifu Mkwawa, maji ya baraka na maajabu ya asili ya kipekee. Mpanga-Kipengere ni hazina ya Taifa letu. Sasa ni jukumu letu kama mabalozi kuutangaza urithi huu Kwa dunia nzima " alisema Nais Sayona ambaye ni mshindi wa Miss Universe Tanzania 2025.
Mbali na kukiri kujifunza mengi katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Mashindano hao nchini, Millen Happiness Magesa alisema mshindi wa shindano hilo atabeba kipande cha makala ya ziara hiyo na kukipeleka katika mashindano ya dunia yanayotarajiwa kufanyika Thailand huku akisisitiza kuwa hiyo ni nafasi ya kipekee ya kuitangaza Tanzania kupitia hifadhi hiyo.Kwa upande wake, Afisa Utalii Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ananias Lugendo alisema Serikali imewekeza katika maboresho ya miundombinu ya hifadhi hiyo ili kuifanya iweze kufikika kwa urahisi zaidi. Aliongeza kuwa uwepo wa mazao mengi ya kiutalii unachangia kuifanya kuwa na mvuto wa kudumu mwaka mzima.
"Hifadhi hii inajivunia kuwa na zaidi ya maporomoko 53 yakiwemo aina 13 kati ya 14 zinazopatikana duniani ambapo maporomoko ya Kimani yamekuwa kivutio kikuu na sasa kupitia walimbwende hawa itapata hadhi ya kimataifa " alisema Lugendo.
Naye Afisa Utalii wa Hifadhi hiyo, Pendo Kimaro alisema ujio wa walimbwende hao ni hatua kubwa ya kuitangaza hifadhi hiyo Kimataifa kupitia majukwaa yao ya Kitaifa na Kimataifa.
"Tunataka ulimwengu ujue kuwa Tanzania ina maajabu, sio tu wanyamapori bali ina hazina ya kipekee yenye mvuto wa kiasili" alisema Kimaro.Ziara hiyo ilifanyika kuanzia Agosti 27, 2025 ikihusisha walimbwende kumi bora wa Mashindano ya Miss Universe Tanzania 2025 wakiongozwa na mshindi wa taji hilo Bi. Nais Sayona.
Washiriki hao walipata fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vya hifadhi hiyo ikiwemo historia ya Chifu Mkwawa, bustani ya dunia, eneo la "massage" ya asili, tafakuri ya kina, matembezi ya mwituni, kuoga mvuke na maporomoko makubwa ya Kimani yenye urefu za zaidi ya mita 250.
No comments
Post a Comment