Zinazobamba

TLP KUZINDUA KAMPENI SEPTEMBA 4 ,MWAKA HUU JIJINI DAR ES SALAAM.

Na Mwandishi Wetu 

Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kimetangaza kuwa kitazindua rasmi kampeni zake za Uchaguzi Mkuu Septemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam, huku kikiahidi kuwa kampeni hizo zitakuwa za kistaarabu, bila vurugu na zenye kujikita katika sera na hoja.

Taarifa hiyo imetolewa na mgombea urais wa chama hicho, Yustas Rwamugira, wakati akizungumza na wanachama na wafuasi wa TLP waliokusanyika katika makao makuu ya chama hicho Magomeni, jijini Dar es Salaam, August.29, 2025.

 Hafla hiyo ilikuwa ni sehemu ya mapokezi yake akitokea jijini Dodoma baada ya kuteuliwa rasmi kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi ujao.

Rwamugira alisema chama hicho kimejipanga kuzunguka nchi nzima kusaka kura kwa wananchi na kutoa elimu ya sera zao, akibainisha kuwa TLP haitabaki kuwa chama cha kushiriki tu bali kimejipanga kwa nguvu zote kuchukua usukani wa kuongoza taifa hili. 

Aliongeza kuwa sera zao zinajikita katika kuimarisha uchumi wa wananchi wa kipato cha chini, kuondoa ukosefu wa ajira, kuboresha elimu na afya, na kulinda rasilimali za taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, mgombea mwenza wa chama hicho alisema atahakikisha maslahi ya haki na usawa wa kijinsia yanalindwa, kwa kuweka mikakati ya kuboresha mazingira ya wanawake kushiriki ipasavyo katika nafasi mbalimbali ndani ya jamii, ikiwemo za uongozi wa kisiasa, uchumi na kijamii. 

Alisisitiza kuwa TLP inatambua mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo ya taifa, hivyo serikali yake itakayoundwa italipa kipaumbele suala hilo kama sehemu ya ajenda kuu za chama.

Aidha, viongozi hao waliwahimiza wanachama na wafuasi wa TLP kuepuka vitendo vya uchochezi au lugha za kejeli wakati wa kampeni, badala yake washiriki katika siasa za heshima na hoja, ili kuonyesha mfano wa siasa safi na zenye kuleta mshikamano wa kitaifa.

Kampeni za Uchaguzi Mkuu zilianza rasmi Agosti 28, 2025 na zinatarajiwa kufungwa Oktoba 28, siku moja kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

No comments