Zinazobamba

PROF.LIPUMBA ATAKA HOTUBA YA WAZIRI MKUU YA BAJETI YA SERIKALI ITOE UFAFANUZI JUU YA MALENGO YA MPANGO WA TATU WA MAENDELEO.


Na Mwandishi Wetu.

Mwenyekiti wa  Chama Cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba amesema kuwa hotuba ya Waziri Mkuu kuhusu bajeti ya Serikali itoe ufafanuzi wa kwa nini malengo ya mpango wa tatu wa maendeleo  hayajafanikiwa licha ya kuwepo mikakati mingi ya utekelezaji.

Profesa huyo wa uchumi pia ameshauri hotuba za Mawaziri wa Sekta nazo zijikite katika kuwaeleza Watanzania sababu za kushindwa kwa Serikali kutekeleza Mpango wa Tatu  wa  Maendeleo katika Sekta zao.

Halikadhalika amesisitiza hotuba hizo za bajeti mwaka huu zichambue sababu za kutofanikisha malengo ya Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo.

" Utaratibu wa zamani wa hotuba za Bunge la Bajeti ulianza na hotuba za Waziri wa Mipango na Waziri wa Fedha kueleza hali ya uchumi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo na mapendekezo ya mapato na matumizi,hivi sasa hotuba hizi ni za mwisho katika Bunge la bajeti,

anayefungua dimba ni Waziri Mkuu ambaye anaeleza utekelezaji wa mipango ya serikali kwa ujumla, hivyo ni vema akaanza kuwaeleza wananchi kwa nini Serikali imeshindwa kutekeleza Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo"amesisitiza 

Amesema hayo, Aprili 6, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa  mtazamo wa chama chake kuhusu bajeti ya mwisho ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo 2021/22 hadi 2025/26.

Amesema kuwa kikao cha Bunge la Bajeti kinatarajiwa kuanza Aprili 8, 2025 na kwamba hii itakuwa bajeti ya mwisho ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo 2021/22 – 2025/26 na mwaka wa mwisho wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. 

Prof.Lipumba amebainisha kwamba hotuba za bajeti, Waziri mara kwa mara hueleza kuwa Bajeti ya Serikali imeandaliwa kwa kuzingatia,Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025,ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26).

Pia imezingatia dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2050, agenda ya Maendeleo ya Afrika 2063,malengo ya maendeleo endelevu 2030; pamoja na nyaraka, miongozo na makubaliano mengine ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Kutokana mlolongo wa nyaraka hizo Profesa Lipumba amefafanua kuwa bajeti inayozingatia mlolongo wa nyaraka nyingi ni wazi haiongozwi na Mpango wa Maendeleo.

Amesema kuwa Machi 11, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na uwekezaji,Prof. Kitila Mkumbo, aliwasilisha Bungeni mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/26. 

Pia Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameki Nchemba naye aliwasilisha Bungeni mapendekezo ya mfumo na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 ambapo Serikali inapanga kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 57.04 kwa mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 13.4 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 ya shilingi trilioni 50.29.

Kwamba Serikali inatarajia kukusanya shilingi trilioni 40.97 kutoka vyanzo vya ndani,ikiwa ni asilimia 69.7 ya bajeti yote ambapo Shilingi trilioni 16.07, sawa na asilimia 30.3 ya bajeti, zinatarajiwa kupatikana kupitia mikopo ya ndani na nje. 

Amesema kuwa Waziri wa fedha ametumia mfumo uliopendekezwa na Shirika la fedha la Kimataifa (IMF) la namna ya kuwasilisha takwimu za fedha za Serikali.

Hata hivyo ameshauri  wakati wa kuwasilisha bajeti Bungeni, Waziri wa fedha atumie mifumo yote miwili kwani uchambuzi wa bajeti katika nchi zinazoendelea umejikita katika kubainisha bajeti ya matumizi ya kawaida na bajeti ya maendeleo. 

"Ukiangalia hotuba ya Waziri wa Fedha iliyowekwa kwenye tovuti ya Bunge na tovuti ya Wizara ya Fedha ni ya PDF iliyowekewa usimbaji fiche (encryption) kwa hiyo huwezi kutengeneza nakala ya hotuba kwa mfumo kuweka kwenye mfumo wa word au excel ili kurahisisha uchambuzi wa bajeti,hivyo namshauri Waziri wa Fedha asitumie usimbaji fiche kwenye nakala ya Hotuba yake ya Bajeti na kwenye Vitabu vya Bajeti,"amesema

Nakuongeza kuwa " Prof. Mkumbo ameeleza kuwa Serikali imetenga  trilioni 19.47 kwa miradi ya maendeleo, ikiwemo Tsh trilioni 13.32 kutoka vyanzo vya ndani na Tsh trilioni 6.15 kutoka nje ambapo Matumizi kwenye miradi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa asilimia 34.1 ya matumizi yote ya serikali.

Mwenyekiti huyo wa CUF Taifa ameendelea kusema kuwa Waziri wa Fedha alieleza Malengo ya Uchumi kwa ujumla kuwa ukuaji wa uchumi umefikia asilimia 6 mwaka 2025 kutoka asilimi 5.4 mwaka 2024 ,ambapo mfumko wa bei ni kati ya asilimia 3.0 hadi 5.0 

Pia mapato ya ndani kufikia asilimia 16.4 ya pato la Taifa mwaka 2025/26 ukilinganisha na matarajio ya asilimia 15.8 mwaka 2024/25,nakwamba mapato ya kodi kufikia asilimia 13.1 ya pato la Taifa mwaka 2025/26 ukilinganisha na matarajio ya asilimia 12.8 mwaka 2024/25.

Hakuna maoni