Zinazobamba

Dr.Philip Mpango mgeni rasmi tuzo ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu.


Na Mwandishi Wetu.

Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu  inatarajiwa kutolewa Aprili 13,2025 ikiwa ni kumbukizi ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere,huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alipozungumza na Waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam,nakubainisha kuwa mshindi wa tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, 2025 ataondoka na kitita cha Shilingi milioni 10, taslimu pamoja na cheti.


Pia mshindi wa pili atazawadiwa  kitita cha Tsh. milioni  7,huku mshindi wa tatu ataondoka na Tsh. milioni 5 na washindi wanne hadi wa 10 watapata cheti pekee.


Prof.Mkenda amebainisha  kwamba maandalizi yote yamekamilika kwa asilimia kubwa na kinachosubiriwa na siku hiyo ya tukio kubwa kufika.


Aprili 13 kila mwaka ndio siku ya kumbukizi ya kuzaliwa, Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere na ndio imepangwa kufanyika kwa tuzo hiyo na huu ni msimu wa tatu.


 

"Mgeni rasmi kuwa ni makamu wa Rais inadhihirisha namna Serikali inavyotambua na kuweka uzito katika tuzo hiyo ya Uandishi Bunifu ambayo kwa njia moja ama nyingine inasaidia kukuza lugha ya Kiswahili kutokana na Waandishi shindani kutumia lugha hiyo katika kazi zao" amesema.


Profesa Mkenda amesema kuwa Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ni miongoni mwa njia bora za kuenzi fikra,falsafa na maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye aliweka msingi wa matumizi na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya elimu, umoja na maendeleo ya jamii ya Watanzania.


“Tuzo hii ni heshima kwa Mwalimu Nyerere lakini pia ni jukwaa mahsusi kwa waandishi chipukizi na wakongwe kuonesha umahiri wao katika nyanja mbalimbali za uandishi kama vile riwaya, ushairi, hadithi za watoto na tamthiliya,” amesema.


Pia amesema mshindi wa kwanza licha ya kushinda Tsh.milioni 10, kazi yake itachapishwa  na kutumika katika shule na maktaba nchini kwa ushirikiano na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hiyo  Profesa Penina Mlama amesema  kwamba majaji wamekamilisha kazi ya kusoma na kuchambua miswaada  iliyowasilishwa na tayari orodha teule ya waandishi waliopendekezwa imechapishwa. 


Profesa Mlimani ameongeza kuwa hadi sasa tayari zimechapishwa kazi mbili za washindi na kazi ya tatu ipo katika hatua za mwisho kukamilika.

Hakuna maoni