SERIKALI KUJENGA ARENA YA WASANII
Serikali imesema itajenga Arena yenye uwezo wa kuingiza zaidi ya watu 15,000 katika eneo la Kawe Dar es Salaam,ili kuondoa changamoto zinazowakumba wasanii wakati wa uandaaji wa kazi zao.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Serikali Greyson Msigwa baada ya msanii wa muziki wa kizazi kipya Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuharakisha ujenzi wa Arena hiyo ili wasanii wapate ukumbi wa kufanya shughuli zao.
Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amewambia Waandishi wa habari Jijini Dar es salaam kuwa baada ya Rais Samia kufanya ziara Korea, amepata mkopo wa masharti nafuu wa Dola bilioni 2.5,kiasi cha fedha hizo zitatumika kwenye ujenzi wa Arena hiyo.
"Kati ya fedha hizo ameamua kukata Shilingi bilioni 450 kwa ajili ya kuzileta Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kujenga Arena kwanza halafu itafuatia kijiji cha filamu,”amesema Msigwa
Nakuongeza kuwa fedha zitakapotoka Korea na kufika kwetu tutaanza ujenzi wa Arena mara moja ili uwanja huo uanze kutumika kwa ajili ya shughuli za michezo na burudani."
“Ndugu zangu Waandishi wa habari Arena inakuja, ndugu zangu wasanii tumshukuru sana Rais Samia, hili jambo lilikuwa linamuumiza kichwa, tutajenga pale Kawe na eneo lilikuwa linaandaliwa linatusubiri sisi,”amesema.
Nakusisitiza kuwa,"namuelewa rafiki yangu Diamond, mimi ameniambia mara nyingi aliniambia nyie mnajenga viwanja lakini sisi mnatusahau, hatimaye tumepata fedha za kujenga,niwapongeze wasanii wote kwa kufanya vizuri,”
Msigwa amesema uwanja huo utakuwa unatumika kwa shughuli nyingine mbalimbali ikiwemo maombi ya kitaifa, mashindano ya Quran na mambo mengine.
Hata hivyo amesema Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) halipendezwi namna wanavyotumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya shughuli za nje ya michezo.
“Inawaudhi kwasababu wanaona viwango vya ubora wa uwanja vinaharibiwa,lakini kwasababu hatuna mahali pengine pa kufanyia shughuli hizi,Arena itasaidia kuondokana na haya,”amesema Msigwa mbele ya Waandishi wa habari.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni