Zinazobamba

DC SAME ASIWASITIZA MAAFISA AFYA, WALIMU NA WATENDAJI KUHAMASISHA USAFI WA MAZINGIRA WILAYANI SAME

Maafisa afya, Walimu pamoja na watendaji wa kata na vijiji ndani ya Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, wamesisitizwa kufanya ukaguzi wa kila kaya na kuchukua hatua za kisheria kwa kaya zisizokuwa na vyoo. Lengo ni kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi juu ya usafi wa mazingira na matumizi bora ya vyoo ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, wakati wa kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi wilayani Same. Amesema kuwa elimu na uhamasishaji kwa wananchi kuhusu usafi wa mazingira na matumizi ya vyoo ni muhimu kwa afya ya jamii na kuzuia magonjwa yanayotokana na uchafu (Magonjwa ya mlipuko).

"Niendelee kusisitiza walimu, maafisa afya pamoja na watendaji wa kata na vijiji kufanya ukaguzi wa kila nyumba na kuwachukulia hatua wale watakaobainika kutokuwa na vyoo, Pia utoaji wa elimu kwa wananchi pamoja na uhamasishaji wa matumizi ya vyoo na usafi wa mazingira ni muhimu sana," alisema Mhe. Kasilda.

Aidha, Mhe. Kasilda amewataka watumishi wa sekta ya afya wilayani Same kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi, kujituma, na kuepuka kuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa wananchi au wagonjwa kuhusu utoaji wa huduma za afya. Amesisitiza kuwa uwajibikaji na uadilifu katika sekta ya afya ni jambo la msingi katika kuboresha huduma kwa wananchi.Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander, amesema kuwa katika mwaka 2024, Idara ya Afya imefanikiwa kufikia asilimia 100 ya ukusanyaji wa mapato lindwa. Aidha, utekelezaji wa mkataba wa afya na lishe umefikiwa kwa asilimia 97 ndani ya wilaya hiyo, hatua inayodhihirisha maendeleo katika sekta ya afya.

Hata hivyo, Dkt. Alexander amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa magari manne ya kubebea wagonjwa (ambulance). Magari hayo yanaendelea kutoa huduma katika maeneo tofauti ikiwemo Hospitali ya Wilaya, Hospitali ya Mji, pamoja na kwenye vituo vya afya, ili kuboresha huduma za dharura kwa wananchi wa wilaya ya Same.



Hakuna maoni