Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU 

BARAZA Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) la Chama cha Wananchi (CUF) limesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana dhima ya kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa 2025 unakuwa huru na wa haki, kwa kuhakikisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inakuwa huru kweli na kutoingiliwa na yeyote katika utekelezaji wa majukumu yake. 

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Prof. Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maazimio ya kikako cha BKUT kilichofanyika Januari 8 Mwaka huu.

"Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limejadili kuhusu Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2025 ndani ya Chama na kwa Taifa kwa ujumla. Kilichotokea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kimeondoa matumaini ya kuwa na Uchaguzi Huru na wa Haki na kuongeza wasiwasi wa kujirudia yale yaliyotokea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020," amesema Prof. Lipumba na kuongeza,

"BKUT linamkumbusha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwamba haki ndiyo msingi na mlinzi wa kweli wa amani kokote duniani,".

Hivyo amesema ni wakati muafaka sasa kutumia utaratibu wa Kisheria kuziba nafasi yoyote iliyo wazi kwenye tume hiyo, kwa kuzingatia Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. 

Kwamba Rais Dkt. Samia ana wajibu wa msingi wa kuwahakikishia Watanzania mapungufu yaliyojitokeza kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Vijiji na Vitongoji 2024 na chaguzi zilizotangulia hayatajirudia kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025. 

"Hili ni muhimu sana likafanyika kwa matamko ya mara kwa mara yanayoahidi kwa dhati dhamira ya kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unakuwa huru na wa haki, ili kuwarudishia matumaini wananchi waliokatishwa tamaa kutokana na kuvurugwa kwa chaguzi zilizopita," ameongeza Prof. Lipumba na kusisitiza,

"CUF Chama Cha Wananchi kinaamini kwamba Uchaguzi Mkuu wa 2025 ndiyo turufu iliyobaki kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwathibitishia Watanzania kwamba ahadi zake za kuwarudisha Watanzania pamoja kupitia Maridhiano chini ya Falsafa ya 4R zilitoka moyoni na si mdomoni tu,".amesema.

Amesema vyovyote iwavyo, hakuna uwezekano wa kufanikisha Maridhiano na kurudisha umoja wa dhati baina ya Watanzania kama Uchaguzi hautakuwa huru na wa haki.

Katika hatua nyingine Baraza hilo lilipokea na kujadili video clip yenye maneno ya Hujuma na Usaliti kwa Chama, yaliyotolewa na Mbunge wa Mtambile kupitia CUF-Chama Cha Wananchi aliyoyatoa mbele ya vyombo vya Habari.
Kwamba Seif aliwaahidi viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba atahakikisha CCM inashinda na kuchukua Jimbo la Mtambile kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kwamba kwake CCM ni kama JAHAZI anayolazimika kuipanda ili asiangamie. 

Pro. Lipumba amebainisha kuwa maelezo hayo yalitafsirika kama hujuma na usaliti kwa Chama na kupelekea Seif aitwe kwenye Kikao cha BKUT cha Januari 8, 2025 kuja kujitetea kutokana na makosa hayo. 

Hivyo BKUT lilijadili makosa hayo,  mwenendo wa jumla wa  Mbunge huyo na dharau yake kwa Chama ikiwa ni pamoja na kutoheshimu wito halali wa kuja kujitetea mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa. 

"Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limekubaliana kwa kauli moja kumfukuza uanachama Mhe. Seif kwa mujibu wa Ibara 83 (4) na 83 (5) za Katiba ya CUF-Chama Cha Wananchi ya mwaka 1992, Toleo la 2019," amebainisha Prof. Lipumba.

Kuhusu uchaguzi wa Katibu Mkuu amesema Baraza hilo lilipokea mapendekezo ya Mwenyekiti wa Chama Taifa ya majina mawili Ali Rashid Abarani na Husna Mohammed Abdallah kupigiwa Kura kwa nafasi ya hiyo, kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 94(1)(m). 
Kwamba BKUT limemchagua Husna Mohammed Abdallah kuwa Katibu Mkuu wa sita (6) wa Chama ambapo Husna anaweka rekodi ya kuwa Katibu Mkuu wa Kwanza mwanamke wa CUF- Chama Cha Wananchi.
Kwa upande wa uchaguzi wa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Baraza hilo lilipokea mapendekezo ya Mwenyekiti wa Chama yaliyotolewa kwa mujibu wa Ibara ya 94 (1)(m), ya wagombea wa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu kwa kila upande wa Muungano. 

Kwamba Anna Ryoba Paul na Magdalena Hamisi Sakaya walipendekezwa kwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara na kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar walipendekezwa Ali Juma Khamis na Leila Jabiri.  
Hivyo Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limemchagua Magdalena Hamisi Sakaya kuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara na Ali Juma Khamis kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.