NAIBU WAZIRI NDERIANANGA ASHIRIKI DUA YA KUMUOMBEA MAREHEMU MHE. JAJI MWANAISHA KWARIKO
NA. MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga ameshiriki dua maalum ya kumuombea marehemu Mheshimiwa Mwanaisha Athumani Kwariko, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (INEC) Tarehe 29 Disemba, 2024 nyumbani kwake Masaki Jijini Dar es Salaam.Dua hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Profesa Ibrahim Juma, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila, Naibu Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. James Henry Kilabuko, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Mhe. Jaji George Kazi pamoja na baadhi ya wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania akiwemo, Mhe. Asina Omari na Mhe. Balozi Omary Mapuri.Akitoa salamu wakati wa dua hiyo Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Profesa Ibrahim Juma ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliofikwa na msiba huo huku akiwakumbusha kuendelea kuishi kwa upendo, amani na utulivu hasa katika kipindi kigumu cha msiba huo.
“Mahakama tutamkumbuka kwa mchango wake hasa uchapakazi wake, tuyaishi aliyoyaacha na tuendeleee kuwa wamoja, na tusisahau maisha yetu si yetu binafsi tuishi kwa ajili ya wengine kama Mhe. Jaji ambaye aliishi kwa ajili ya wengine hakika ametuachia somo,” alisema Mhe. Prof. Juma
Aliongezea kuwa watamkumbuka kwa namna alivyotenda haki na kuongoza kwa weledi na upendo, huku akikumbusha kuendelea kumuabudu Mungu katika uhai tuliopewa.
“Uwapo kazini jua wewe ni kiongozi katika eneo lako la kazi, hivyo tujifunze kutenda haki mahali tulipo, tusiache kutenda wema, maana unapowekwa mahali una nafasi ya kuongoza wengine,” alisisitizaAidha, Marehemu Jaji Mwanaisha anatarajiwa kuzikwa tarehe 30 Disemba, 2024 katika kijiji cha Bicha Wilaya Kondoa Jijini Dodoma
Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu
Hakuna maoni
Chapisha Maoni