Zinazobamba

WAKULIMA LINDI WATAKIWA KUFUATA USHAURI WA KITAALAMU KWENYE KILIMO

Na Mwandishi Wetu,Lindi

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuachana na maneno ya kusikia kutoka kwa watu wanaowaaminisha kuwa mbolea inaharibu udongo badala yake wafuate ushauri unaotolewa na wataalam wa kilimo ikiwemo kutumia mbolea kwa usahihi kwenye shughuli zao za kilimo.

Ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni inayotekelezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ya Kilimo ni mbolea uliofanyika katika kijiji cha Mandawa wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi yenye lengo la kuwaelimisha wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na kuhamasisha usajili wa wakulima kwenye mfumo wa kidijitali wa mbolea za ruzuku.

"Wananchi tubadilike yapo maneno yanasema ukitumia mbolea unaharibu udongo, mbolea ingekuwa inaharibu udongo mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wanaolisha nchi nzima nasisi tukiwepo wasingekuwa wanazalisha mpaka sasa"

Hayo maneno tunayoyaamini kutoka kwa watu wasiokuwa na utaalam, hawajaenda shule tuachane nayo, tunatumia nguvu kubwa ya kulima eneo kubwa wakati matumizi ya mbolea yangetufanya tulime eneo dogo kwa matokeo makubwa" Nyundo alisisitiza.

Alisema,  Sisi tunao maafisa kilimo kwenye ngazi ya Mkoa,  Wilaya, kata na vijiji na kueleza maafisa hao wanaujuzi unaofanana na kuwataka wakulima kuwatumia hao ili kushauriwa namna bora ya kulima mazao yao. 

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilwa, Farida Kikoleka amesema, huko nyuma suala la kilimo lilikuwa kama adhabu ila kwa sasa wananchi wamebadilika na wanajua kuwa kilimo ni chakula lakini pia wanajua kilimo ni biashara.

Amesema, kufuatia mwitikio mkubwa wa wananchi waliohudhuria  hafla hiyo kuwa mabalozi wa kufikisha ujumbe na elimu ya mbolea waliyoipata  kwa wakulima waliokosa fursa hiyo.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kilwa, Mbaruku Masudi ameipongeza TFRA kwa kuja na wazo na kuamua  kushuka hadi  ngazi ya wakulima ili kuwapa elimu muhimu ya mbolea. 

Ameiomba Mamlaka kuwa na nia ya kuwafikia wakulima wa kata nyingine ambao hawakufanikiwa kushiriki hafla hiyo ya uzinduzi. 

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TFRA, Robert Mtendamema ametoa shukrani kwa uongozi wa Mkoa na wilaya kwa kushirikiana kikamilifu katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kupitia kampeni hiyo.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya kilimo imekusudia Sekta ya kilimo kukua kwa asilimia kumi ifikapo mwaka 2030 na kueleza matumizi sahihi ya mbolea yatachangoza kufikiwa kwa lengo hilo kwani wakulima watazalisha kwa tija na kuongeza vipato vyao na taifa kwa ujumla.



Hakuna maoni