Zinazobamba

HESLB NA TRA KUSHIRIKIANA KUWABAINI WANUFAIKA WA MIKOPO WALIO SEKTA ISIYO RASMI

Na Mussa Augustine 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu nchini,(HESLB) imebadilishana hati za ushirikiano baina yake na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),ikiwa ni muendelezo wa kuboresha huduma zake  kuwafikia wanufaika wa mikopo hiyo.

Akizungumza leo Septemba 13,2024 Jijini Dar es salaam  wakati wa  hafla fupi ya kubadilishana hati za ushirikiano huo ,Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt.Bill Kiwia amesema kuwa lengo la kushirikiana na TRA ni kuwafikia wanufaika wa mikopo walio katika sekta isiyo rasmi ambao wana kipato na hawajarejesha mikopo yao.

Dkt.Kiwia amesema kwamba  kupitia ushirikiano huo, HELSB  itaboresha huduma zake kwa urahisi na kuwafikia wanufaika wa mikopo kupitia kanzidata za TRA ambao watatoa taarifa za wanufaika wa mikopo ambao hawajairejesha nakuweza kuwachukulia hatua ili wanufaika wengine walio vyuoni nao waweze kupata Mikopo hiyo.

"Jambo  tunalolifanya hapa leo litachangia sisi HESLB na TRA kubadilishana uzoefu baina yetu na kuwafanya wale wasiorejesha mikopo yao ambao hawapo kwenye ajira rasmi lakini wana kipato kupitia sekta isiyo rasmi,kurejesha Mikopo"amesema Dkt Kiwia

Aidha ametoa wito kwa  wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao bado hawajaanza kurejesha Mikopo yao,kurejesha kwa wakati ili kufanya bodi hiyo kuwa na uwezo wa kutoa Mikopo kwa Wanufaika wengine.

Nae  Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Yusuph Mwenda ameipongeza bodi hiyo kwa kazi kubwa ya utoaji mikopo kwa wanafunzi wa kitanzania ambayo imechangia pakubwa katika kukua kwa sekta ya elimu nchini.

"Kile mnachokifanya  Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu ni Matokeo ya watanzania kulipa Kodi na hatimaye kodi hizo pia kutumika kugharamia bodi katika utoaji mikopo kwa watoto wetu wa kitanzania" amesema

Aidha Kamishna Mwenda amesema kuwa TRA itakuwa mstari wa mbele kubadilishana taarifa na bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu(HESLB) ili kuhakikisha wanufaika wa mikopo ambao wako sekta isiyo rasmi wanarejesha mikopo hiyo.

HELSB imekua ikishirikiana na wadau mbalimbali wa Kimkakati ili kuhakikisha wanaleta ufanisi mkubwa  katika utoaji wa Mikopo ya Elimu ya Juu kwa Watanzania.

Hakuna maoni