Zinazobamba

KITANZI CHA KIBOKO YA WACHAWI CHAMUIBUA KOMANDO MASHIMO


Na Mussa Augustine 

Mchungaji wa Kitaifa Nabii Komando Mashimo ameiomba Serikali Kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuifungulia huduma ya Kanisa la huduma ya kinabii linaloongozwa na Nabii Kiboko ya Wachawi lililopo Buza kwa Lulenge Mkoani Dar es salaam.

Rai hiyo ameitoa leo Agost 2 , 2024 kanisani hapo wakati akizungumza na Waandishi wa habari ambapo amesema kwamba serikali ilipaswa kutoa onyo kabla ya kanisa lake kufungwa,hivyo ameiomba serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan kuifungulia huduma hiyo kwani imewasaidia Wananchi wengi  kuondokana na changamoto mbalimbali kwenye maisha yao.

Aidha Mashimo amesema kwamba kufungiwa kwa kanisa hilo serikali haijahusika moja kwa moja bali ni hila zilizofanywa na baadhi ya watu kutokana na Mchungaji Dominick "Kiboko ya Wachawi"kwa muda mfupi kupiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma zake za kiroho.

Hata hivyo kwa Mujibu wa Mashimo amesema kuwa uongozi wa kanisa hilo unatarajia kukata rufaa kutokana na kufungiwa kwa kanisa hilo nakwamba ana aamini serikali itatenda haki kama endapo hakutakua na sababu nyingine nyuma ya sakata hilo.

Kwa Upande Wake Mchungaji Msaidizi wa Kanisa hilo Mch.Athanas Christopher amesema kwamba sababu zilizopelekea kufungwa kwa kanisa hilo niza uongo na zimepangwa kwa ajili ya kukwamisha huduma za kanisa hilo."

Sababu ambazo wanasema kwamba eti waumini wanatozwa pesa nyingi kumuona mtumishi wa Mungu,ni uongo kwani waumini wanaosali hapa kwa ibada moja ni zaidi ya elfu nane,sasa ina maana hawa wote hawana akiri kweli? amehoji Mchungaji huyo.

Aidha amesema  kwamba kufungiwa kwa kanisa hilo kumeathiri shughuli za kiuchumi kwa Vijana na wakina mama, kwani Vijana walikua wanatoa huduma za usafiri wa Bodaboda na bajaji kwa waumini huku wakina mama wakitoa huduma mbalimbali ikiwemo chakula na vinywaji.

Baadhi ya Waumini wa Kanisa hilo akiwemo Carolina Mushi na Mjuni Mtahaba wameiambia Fullhabari kuwa kufungiwa kwa kanisa hilo kumewaumiza kifikra kwani wao wamefanikiwa kuondokana na matatizo ambayo yalikua yanawasumbua kabla ya kuanza kupata huduma katika kanisa hilo."

"Tunaiomba serikali imfungulie mtumishi wetu,baba yetu Kiboko ya Wachawi kwani sisi ndio tunaemuamini kutokana na kutufungua katika changamoto mbalimbali ikiwemo magonjwa,na Uchumi wetu,sisi hapa hatujalazimishwa na mtu,tunatoa  pesa kwa ajili ya kukamilisha ibada tunayopata,kusema kwamba tunatozwa Fedha nyingi kumuona Mtumishi ni uongo,tunatoa wenyewe kwa kupenda" wamesema Waumini hao kwa nyakati tofauti.

 Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia kwa Msajili wa Asasi za kirai ,ilifungia huduma za kanisa la Kiboko ya Wachawi kwa madai kuwa linatoa mahubiri chonganishi kwa jamii nakupelekea kuleta taharuki kwa baadhi ya makanisa yanayotoa huduma kama hizo hapa Nchini.


Hakuna maoni