Zinazobamba

WHI KUANZA UJENZI WA NYUMBA 101 DAR ES SALAAM,MRADI UNAGHARIMU KIASI CHA SHILINGI BILIONI 18.6

Na Mussa Augustine

Watumishi Housing Investment (WHI) imetiliana saini na Mkandarasi Shadong Hi-Speed Group kutoka China kwa ajili ya Utekelezaji wa Ujenzi wa Jengo la Gholofa 12 lenye  Nyumba 101 ,ambazo zitajengwa katika eneo la Mikocheni Regent Estate Jijini Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini huo leo Julai 30,2024 Jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment Dkt Fred Msemwa amesema kwamba ujenzi huo utaanza rasmi Mwezi Agost Mwaka huu, na utakamilika ndani ya miezi 18."Ujenzi huu  utagharimu kiasi cha  shilingi bilioni 18.6 ikiwemo pamoja na Kodi ya Ongezeko la thamani( VAT )lakini bila VAT  mradi huu nagharimu shilingi bilioni 15 pekee" amesema Dkt Msemwa mbele ya Waandishi habari.

Aidha amesema kwamba ujenzi huo wa Mradi wa kisasa  umezingatia uwepo wa miundombinu ya kisasa ikiwemo miundombinu ya Maji na Umeme ili kuhakikisha watumishi watakaonunua Nyumba hizo hawapati changamoto za ukosefu wa huduma muhimu za  Maji na Umeme.

" WHI tayari imejenga Nyumba 1003 katika mikoa 19 Nchini Tanzania na Nyumba 101 ambazo utiaji saini na Mkandarasi Shadong Hi Speed Group unafanyaika leo ni sehemu ya Nyumba 218 zitakazojengwa katika Mikoa ya Dodoma,Lindi,Mtwara,Singida ,Pwani,na Ruvuma katika Mwaka wa Fedha 2024 /2025" amesema Dkt Msemwa.

Nakuongeza kuwa " Nyumba hizi zitauzwa kwa utaratibu maalumu wa unafuu kwa watumishi wa Umma,bei ya Nyumba ya chumba kimoja chenye sebule,chumba Cha kulala,choo,stoo ,jiko na balcony nakadhalika itaanza shilingi milioni 99 na Bei ya Nyumba ya vyumba vitatu vya kulala ,sebule,stoo,balcony itaanzia shilingi milioni 234".

Aidha Dkt Msemwa amesema kuwa bei ya Nyumba hizo zikilinganishwa na Nyumba za aina hiyo katika eneo la Mikocheni ,Nyumba hizo ni nafuu kwa kati ya asilimia 10, hadi asilimia 40 ,nakwamba uuzaji wa Nyumba hizo tayari umeanza na WHI inatarajia kuwepo kwa mwitikio mkubwa kutoka kwa walengwa.
Kwa Upande Wake Msaidizi wa Kampuni ya Shadong Hi- Speed Group, Li Guangdang ameshukuru kupata zabuni hiyo huku akiahidi kutekeleza Mradi huo kwa mujibu wa Makubaliano ya mkataba.

"Kwaniaba ya Kampuni napenda kushukuru kwa kupata zabuni hii,tutatekeleza Mradi huu kwa kufuata Makubaliano yakimkataba,na pia hii ni fursa kubwa kwetu yakuendelea kutangaza Kampuni yetu kimataifa" amesema Li

Watushi Housing Investment ni taasisi ya Umma chini ya Ofisi ya Rais Utumishi yenye jukumu la uendelezaji wa milki na usimamizi wa uwekezaji kupitia uanzishaji na usimamizi wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja ambapo WHI inasimamia mfuko wa Nyumba pamoja na Mfuko wa Faida Fund.





Hakuna maoni