ASILIMIA 90 YA WATANZANIA BADO WANATUMIA NISHATI AMBAYO SIO RAIFIKI, SERIKALI YAZINDUA MKAKATI WA TAIFA MATUMIZI NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassan amesema kuwa
asilimia 90 ya watanzania bado wanatumia Nishati ambayo sio rafiki, huku
akisisitiza umuhimu wa kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya
Nishati Safi ya Kupikia ili kufikia malengo ya asilimia 80 ya Watanzania
kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Dkt.Samia
ameyasema hayo leo Mei 8, 2024 jijini Dar es Salaam akizungumza katika hafla ya
Uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, iliyofanyika
katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Aidha ametumia
fursa hiyo kuitaka Wizara ya Nishati kukaa na wadau ili kubaini maeneo ambayo
yakifanyiwa maboresho yatasaidia upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa wakati umefika kwa sekta binafsi nchini kuongeza uwekezaji na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka kuleta teknolojia rahisi
itakayowezesha wananchi kupata nishati safi kadri ya uwezo wao pamoja na
kulipia kulingana na matumizi kama inavyofanyika katika umeme.
Amesema kuwa lengo la Mkakati huo likitekelezwa na kutimia
litapunguza gharama ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuongeza upatikanaji
na uwekezaji wa nishati safi.
Rais Samia amebainisha kuwa Mkakati huo wa kitaifa pia utachangia
jitihada za Serikali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana
na uharibifu wa misitu ambao huchangiwa na shughuli za kibinadamu.
Amesema kuwa kwa sasa, inakadiriwa kuwa takribani hekta 469,000 za
misitu hupotea kila mwaka ambapo nishati za kuni na mkaa ni moja ya chanzo
kikuu cha kutoweka kwa misitu hiyo.
Akisoma taarifa ya Makakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi
ya Kupikia,Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa amesema kuwa mradi huo utagharimu
shilling trilioni 4.6 ambao utamudumu kwa muda wa miaka 10 mpaka 2034, huku
akifafanua kuwa umefata sera za Kitaifa na Kimataifa ili kuleta tija.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amesema kuwa lengo la mikakati wa Nishati Safi ya Kupikia ni kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2030 asilimia 80 ya watanzania watumie Nishati Safi pamoja na kusimamia kikamilifu Mkakati huo ili kuleta matokeo ya haraka na kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo, amesema kuwa changamoto iliyopo kwa sasa uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya Taifa ya Nchi, huku akiadi utekelezaji kwa ufanisi.


No comments
Post a Comment