JAMII YANUFAIKA NA TSA

Mkurugenzi wa Kampuni ya Nabii Eliya ameeleza mafanikio makubwa yaliyoleta matumaini na manufaa ya moja kwa moja kwa jamii, hususan kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini.
Akizungumza leo Septemba 26, 2026, katika Siku ya Wachimbaji Wadogo wa Madini na Watoaji wa Msaada wa Kiufundi (TSA), kwenye Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, mkurugenzi huyo alisema kampuni yake imejikita katika kuleta tija na suluhu za kudumu.
Amesema kupitia huduma zao za kiufundi, wachimbaji wengi wameweza kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za uendeshaji na kufanya kazi kwa usalama zaidi
"Lengo letu si biashara tu, ni kuinua mchimbaji mdogo. Tunapompa mchimbaji teknolojia sahihi, tunampa matumaini ya kesho iliyo bora kwa familia yake na jamii yake," alisema Mkurugenzi huyo.
Ameongeza kuwa kampuni yake imefanikiwa kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania kupitia mafunzo ya vitendo migodini, kuingiza teknolojia rafiki inayomwezesha mchimbaji mdogo kuchimba kwa tija bila kuharibu mazingira, pamoja na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii kwa kuchangia huduma za kijamii katika maeneo yanayozunguka migodi.
Kauli yake iliibua shangwe, makofi na vicheko vya furaha kutoka kwa washiriki waliofurahishwa na mwelekeo huo.
Mkutano huo ni sehemu ya maonesho yenye kaulimbiu isemayo Kuwezesha Wachimbaji Wadogo Kuongeza Tija Kujenga Sekta Imara yanayolenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kunufaika zaidi na rasilimali za madini nchini.
No comments
Post a Comment