TANESCO YATOA ELIMU USALAMA WA UMEME LIULA
SONGEA.
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalama wa umeme, hasa katika kipindi hiki cha mvua kubwa zinazotabiriwa.
Akizungumza katika Kijiji cha Liula, Kata ya Matimila, Songea DC, Msaidizi wa Afisa Huduma kwa Wateja wa TANESCO Ruvuma, Emma Ulendo, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari wanapoona nguzo au nyaya za umeme zimeanguka.
Aliwasisitiza kutokaribia maeneo yenye nguzo au nyaya zilizoanguka, bali kutoa taarifa TANESCO ili wataalamu wafike na kuchukua hatua salama.
Pia aliwakumbusha wananchi kutomshika kwa mikono mtu aliyenaswa na umeme, bali kutumia mti mkavu kumsukuma pembeni bila kujihatarisha.
Ulendo aliwafahamisha wananchi kuhusu mradi mpya wa umeme wa REA, akiwataka wanaohitaji kuunganishiwa umeme kuchukua na kujaza fomu ili majina yao yaingizwe kwenye orodha ya wanaosubiri huduma hiyo.
Aidha, aliwakumbusha wananchi kulinda miundombinu ya TANESCO na kuepuka kuchoma moto karibu na nguzo za umeme.
Diwani wa Kata ya Matimila, Mennace Komba, alisema asilimia 98 ya vitongoji vya kata hiyo vimepata umeme na kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kujiongezea kipato.
Alisema baadhi ya shughuli zilizonufaika na umeme ni saluni na uchomeleaji wa magrili, mageti na kazi mbalimbali za chuma.
Kwa upande wake, Inspector Kulwa Charles Kiluka, Polisi Kata wa Matimila, aliwataka wananchi kuwa mstari wa mbele kulinda miundombinu ya umeme na kutoa taarifa kuhusu watu wanaohusika na wizi wa vifaa vya TANESCO.
Wananchi Dickson Tadei Komba, Hamisi Abbas Komba na Moses Luhambano walieleza umuhimu wa elimu hiyo na matumizi salama ya umeme katika jamii.

No comments
Post a Comment