TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA AJIRA AFRIKA,GCC PLUS
DAR ES SALAAM.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Afrika na nchi za Ghuba (GCC Plus),unaojulikana kama "DOHA DIALOGUE II" unaolenga kuimarisha ushirikiano katika uhamaji wa wafanyakazi, ajira na mahitaji ya soko la ajira kati ya nchi za Afrika na Mataifa ya Kiarabu.
Mkutano huo utafanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu na utawakutanisha wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC), ambazo ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain, pamoja na Jordan na Lebanon.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Septemba 28, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja kuhusu uhamaji salama na wenye tija, unaozingatia haki za wafanyakazi, pamoja na kukuza fursa za ajira, hususan kwa vijana.
Sangu amesema mkutano huo ni mwendelezo wa Mkutano wa Kwanza uliofanyika jijini Doha, Qatar, Mei 21 na 22, 2024, ulioshirikisha nchi 43, zikiwemo 25 za Afrika, nchi za GCC pamoja na Jordan na Lebanon, zinazojulikana kwa pamoja kama GCC Plus.
“Tanzania ilishiriki katika mkutano huo wa kwanza ambao ulihusisha majadiliano yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na nchi za Kiarabu katika masuala ya uhamaji wa wafanyakazi,” amesema.
Amesema mkutano huo ulihitimishwa kwa kupitishwa kwa Azimio la Doha (Doha Declaration), lililoweka msingi wa kuendeleza majadiliano na ushirikiano kati ya pande hizo.
Sangu amesema Tanzania imepata nafasi ya kuwa nchi ya pili kuwa mwenyeji wa mkutano huo, ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili, na kwa mara ya kwanza kufanyika katika bara la Afrika.
“Moja ya maeneo muhimu yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni kuimarisha uhamaji wa wafanyakazi kati ya nchi, ikiwemo makubaliano ya uhamaji, ujuzi wa wafanyakazi, mahitaji ya soko la ajira na uanzishwaji wa mifumo ya kusaidia uhamaji salama na wenye tija,” amesema.
Kwa mujibu wa Sangu, mkutano huo pia utajadili namna ya kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira, pamoja na kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.
Amesema kwa Tanzania, mkutano huo utatoa fursa ya kimkakati ya kuimarisha nafasi ya nchi katika mijadala ya kimataifa kuhusu uhamaji wa wafanyakazi, kubainisha fursa za ajira ndani na nje ya nchi, kulinda haki za wafanyakazi na kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika na GCC Plus.
“Mkutano huo unatarajiwa kuongeza ushindani wa wafanyakazi wa Tanzania katika soko la ajira la kimataifa na kuchangia katika utekelezaji wa ajenda za maendeleo ya taifa,” amesema.
Aidha, amesema mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na GCC Plus katika masuala mbalimbali ya uhamaji wa wafanyakazi, huku ukilenga kubadilisha makubaliano na majadiliano yaliyopo kuwa hatua za vitendo na matokeo yanayopimika.
“Kupitia ushirikiano huo, Tanzania inatarajia kuona fursa zaidi za ajira kwa Watanzania, hususan vijana, huku ikiweka mkazo katika uhamaji wa wafanyakazi ulio salama, wenye haki, tija na unaozingatia mahitaji ya nchi na soko la ajira,” amesema Waziri Sangu.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inaamini kuwa mkutano huo utaimarisha ushirikiano na washirika wa kimataifa na kufungua fursa zaidi za ajira kwa Watanzania.


No comments
Post a Comment