Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Ismail Seleman akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba 2023 hadi Desemba 2023.

NA MWANDISHI WETU

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wailaya ya Kinondoni pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni wamebaini Kampuni iliyopewa jukumu la kukusanya ushuru wa masoko ya Manispaa ya Kinondoni imekuwa ikifanya udanganyifu katika ukusanyaji na uwasilishaji wa mabato hayo Benki.

Hayo yamebainishwa leo Februari 6, 2024 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Ismail Seleman akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba 2023 hadi Desemba 2023.

"TAKUKURU kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni tumefanya ufuatiliaji na kubaini kampuni iliyopewa jukumu la kukusanya ushuru wa masoko ya Manispaa ya Kinondoni imekuwa ikifanya udanganyifu katika ukusanyaji wa mapato hayo Benki," amesema Seleman na kuongeza,

"Ofisi yetu ya TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni kwa kipindi cha mwezi Oktoba na Novemba 2023 imefanya ufuatiliaji na uangalizi wa kichunguzi (Observation) kwa muda wa siku 6 na kuthibitisha kuwa Kampuni ya Prezzidar inakusanya na kuwasilisha benki kiasi kidogo kuliko uhalisia wake,".

Seleman ameongeza kuwa wamefanya uchunguzi kuhusiana na mapato hayo na kubaini kuwa watendaji wa kampuni hiyo ya Prezzidar wamekuwa wakihujumu mapato kwa kutumia POS mashine ipasavyo. 

Hivyo amebainisha kuwa Januari 10, 2024 watendaji hao walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni kwa tuhuma za uhujumu uchumi, ubadhirifu, kusaidia kutenda kosa, kuongoza genge la uhalifu na uchepushaji wa mapato ya ushuru ambapo wamefunguliwa kesi Na. 1638/2024.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara wote kuzingatia miongozo inayotolewa na Halmashauri na Serikali kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kulipa ushuru na kuhakikisha wanapatiwa stakabadhi sawa na kiasi walichotoa.

Kadhalika  ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni hususan Idara husika kuhakikisha inasimamia kwa ukaribu wazabuni wote waliopewa dhamana ya ukusanyaji ushuru kwa niaba ya Halmashauri.

Akizungumzia kuhusu uzuiaji rushwa,Ismail amesema katika kipindi husika, wamefuatilia miradi minne (4) yenye thamani ya shilingi 7,234,254,382.23/= ambayo inaendelea na utekelezaji.
Aidha ameongeza kuwa katika miradi hiyo wamebaini kasoro ndogo ndaogo ambazo wahusika wameshauriwa kurekebisha kasoro hizo na kwamba wataendelea kufuatilia kwa karibu hadi miradi itakapokamilika ili kuhakikisha inakamilika kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha.