Waziri Kivuli wa Uchukuzi wa Chama cha ACT Wazalendo Kizza Mayeye (Pichani juu)akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara Halima Nabalang’anya akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kusitisha nauli mpya za mabasi na daladala zilizoanza kutumika tangu mwezi Desemba 2023 na kuitaka Serikali ichukue hatua madhubuti kushusha bei ya sukari inayolalamikiwa na wananchi nchi nzima. 

Hayo yameelezwa  leo Februari 4, 2024 na Waziri Kivuli wa Uchukuzi Kizza Mayeye na Waziri wa Viwanda na Biashara Halima Nabalang’anya wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Kuhusu ongezeko kubwa la nauli mpya za mabasi na daladala Waziri Kizza amesema bei mpya zilizotangazwa na Serikali zimeongezeka kwa wastani wa kati ya Shilingi 270 hadi shilingi 400 kwenye shilingi 1,000 kwa daladala. 

Kwamba kwa upande wa nauli za mabasi amesema ndio imeleta maumivu zaidi kuna mikoa imeongezeka Shilingi 6,000 hadi 17,000 wastani wa asilimia 18 hadi 22.

“Kitendo cha Serikali kuridhia maamuzi ya bodi ya LATRA inaonyesha wazi kabisa haiwajali wananchi wake na kuwatelekeza. Nauli hizi zimeangalia maslahi ya wasafirishaji na si hali za wananchi wa kawaida," amesema Kizza. 

Hivyo Waziri Kizza ametoa wito kwa Serikali kusitisha matumizi ya nauli mpya ili kutoa nafasi kwa LATRA  kufanya marejeo upya na Serikali kufanyia kazi madai ya wasafirishaji kwa kurejesha ruzuku kwenye mafuta na matumizi ya Gesi asilia. 

Kwa upande wa kuhusu kupanda kwa bei ya sukari Waziri Kivuli wa Biashara na Viwanda Halima amesema kauli za Serikali hazijasaidia hata kidogo kutoa nafuu ya bei ya sukari tofauti na ahadi na hadaa inazozitoa. 

Hivyo ameitaka Serikali kwa hatua za haraka iweke nguvu kubwa kuhakikikisha upatikanaji wa kutosha wa sukari ili kuhakikisha bei inashuka na wananchi wanapata sukari kwa wakati na kwa bei nzuri.

“Tunaitaka Serikali kuongeza kasi ya uwekezaji na uzalishaji katika viwanda kwa kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria na kuchochea matumizi ya teknolojia za kisasa," ameeleza Halima.

ACT Wazalendo imesisitiza kuwa kazi kubwa ya Serikali yoyote ile dunia ni kuangalia ustawi wa wananchi wake. Kitendo cha Serikali kutumia hadaa na kuziba masikio juu ya kero za sukari na kupanda kwa nauli tena ndani ya miaka miwili mfululizo kutangazwa bei mpya mara mbili ni kuichora kama Serikali isiyojali.