Zinazobamba

NHIF YAFANYA MABORESHO MAKUBWA YA KITITA CHA MAFAO KWA WANACHAMA WAKE,YAKARIBISHA MAONI YA WADAU

Na Mussa Augustine.

 Mfuko wa Bima wa Taifa wa NHIF imefanya maboresho ya kitita Cha Mafao kwa Wanachama wake ambayo utekelezaji wake utaanza rasmi Machi 1, 2024 ikwa lengo ni upatikanaji wa huduma Bora wa Wanachama pamoja na kuongeza huduma ambazo hazikuepo hapo awali.

 Hayo yamesemwa leo Februari 28,2024 jijini Dar es salaam na  Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt, Benard Konga wakati akizungumza na waandishi wa habari,ambapo amesema kuwa maboresho ya mwisho ya kitita Cha Mafao ya Mfuko huo kinachotumika kwasasa yalifanyika Mwezi June, 2016 na hivyo upo umuhimu wa kufanya marejeo yake kutokana na sababu mbalimbali.

 Aidha Dkt Konga, ameendelea kubainisha kuwa  Maboresho hayo ya Orodha ya huduma za Matibabu ambazo zinatolewa kwa wanufaika wa NHIF na bei zake ambazo hutumika wakati wa malipo kwa madai ya watoa huduma za Matibabu yamezingatia Maendeleo ya teknolojia na hali halisi ya bei katika soko ,pia kuwianisha kitita cha Mafao na Miongozo ya tiba iliyoboreshwa ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanufaika wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

 Mkurugenzi Mkuu huyo wa NHIF kupitia taarifa yake kwa Vyombo vya habari amefafanua kuwa maeneo yaliofanyiwa Mapitio na Maboresho ya kitita cha Mafao ni pamoja na ada ya usajili na kupata ushauri wa daktari,Huduma za dawa, vipimo,upasuaji na gharama za kliniki za kawaida na kibingwa .

 “Jumla ya dawa 736 zimefanyiwa mapitio kwa kuzingatia bei ya soko na gharama za uendeshaji na wastani wa faida ,hii itaondoa changamoto ya wananchi kukosa baadhi ya huduma za dawa kutokana na changamoto ya bei,pia tumeongeza dawa mpya zipatazo 247 ambazo zinatokana na dawa mpya zilizopo kwenye muongozo wa orodha ya dawa muhimu za Taifa (NEMLIT)”amesisitiza  Dkt Konga.

 Nakuongeza kuwa  “Gharama za vipimo 311 na upasuaji zimefanyiwa mapitio kwa kuzingatia bei za soko katika ununuzi wa vifaa na vitendanishi ,gharama za uendeshaji na wastani wa faida hii itaondoa changamoto ya kukosekana  kwa huduma za vipimo na upasuaji kutokana na changamoto ya bei”. 

 Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu huyo amewaomba wananchi kuendelea kujiunga na NHIF ili kuwawezesha kupata huduma za matibabu kupitia Mfuko huo kwani lengo la Serikali ni kuanza kutoa huduma za Afya kuanzia ngazi ya zahanati, hadi hospital ngazi ya Taifa,nakwamba Mpango wa huduma ya afya kwa wote unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

 Kwa mujibu wa Dkt.Konga NHIF  itaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau na itaendelea kuwajulisha pindi maboresho yoyote yatakapotokea ili kuwa na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Hakuna maoni