TEA: Mradi wa kuendeleza ujuzi umekamilika kwa mafanikio, vijana 49,000 wamenufaika
Kaimu
Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Masozi Nyirenda akitoa
elimu kwa wadau waliotembelea banda la TEA wakati wa maonesho ya miaka 50 ya
Baraza la Mitihani la Tanzania yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam viwanja vya
Mnazi Mmoja.
Na Mwandishi wetu-Dar es salaam
Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Masozi
Nyirenda amesema serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imefanikiwa
kukamilisha mradi wa kuendeleza ujuzi kwa mafanikio makubwa ambapo jumla ya
vijana 49,000 wamenufaika kwa kupata ujuzi.
Mh. Nyirenda amesema hayo Novemba 3, 2023 wakati akizungumza na
waandishi wa habari waliotembelea Banda la TEA wakati wa maonyesho ya miaka 50
ya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), yaliyofanyika katika uwanja wa Mnazi
mmoja Jijini Dar es salaam
“Mwaka 2017 TEA ilikabidhiwa jukumu la ziada na Wizara ya Elimu
sayansi na teknolojia kusimamia mfuko wa kuendeleza ujuzi, huu ni mfuko ambao
kazi yake ni kufadhili taasisi zinazotoa mafunzo ya ujuzi pamoja na vijana
ambao wanataka kupata mafunzo hayo, mwishoni mwa mwezi Juni tulikamisha mradi
ambapo vijana elfu 49 walinufaika,” alisema
Vilevile, amesema katika ufuatiliaji walioufanya kwa lengo la
kubaini vijana hao wameishia wapi baada ya kupata ujuzi, wamebaini asilimia 80
wapo kazini, aidha kwa kuajiliwa au kujiajili.
Akieleza kwa nini wameshiriki katika maonesho ya baraza la
mitihani Tanzania, Masozi amesema wao ni wadau wakubwa wa elimu na hivyo ni
muhimu wakakutana na wananchi na kutoa elimu juu ya kazi wanazozifanya
“Wenzetu NECTA wanatathimini ubora wa elimu, sisi tunafadhili
vifaa na kuhakikisha mazingira ya ufundishaji yanakuwa bora, kwa hiyo tupo hapa
kueleza fursa zinazopatikana,” alisema
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa mstari wa
mbele katika kutekeleza, na kusimamia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)
ikiwemo kusimamia upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa kote nchini pamoja na
uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia.
Katika kufanikisha utekelezaji wa malengo haya, Serikali
imeendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya Elimu kuanzia elimu ya
awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu. Maboresho na mageuzi haya yanahitaji
rasilimali na nguvu kazi kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuunga mkono jitihada
za Serikali za kuboresha sekta ya sekta ya Elimu.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inalo jukumu la kuhamasisha
uchangiaji maendeleo ya Elimu kote nchini ambapo, kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko
wa Elimu, Namba 8 ya mwaka 2001 sehemu ya 12 (1) (a) na (b) mchangiaji ni mtu
yeyote anayetoa mchango wa pesa, bidhaa, au huduma kupitia Mfuko wa Elimu wa
Taifa au kutekeleza mradi kwa uratibu wa Mfuko huo wa Elimu
Hakuna maoni
Chapisha Maoni