Wadau wa sekta ya elimu washauriwa kuchangia maendeleo ya elimu kupitia mfuko wa elimu wa taifa
Afisa Miradi kutoka TEA Bi. Mwafatma Mohamed akitoa Elimu kuhusu kazi zinazotekelezwa na TEA katika Maonesho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania Jijini Dar es Salaam |
Na
Mwandishi wetu
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa mstari wa
mbele katika kutekeleza, na kusimamia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)
ikiwemo kusimamia upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa kote nchini pamoja na
uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia.
Katika kufanikisha utekelezaji wa malengo haya, Serikali imeendelea
kufanya maboresho makubwa katika sekta ya Elimu kuanzia elimu ya awali, msingi,
sekondari hadi vyuo vikuu. Maboresho na mageuzi haya yanahitaji rasilimali na
nguvu kazi kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuunga mkono jitihada za Serikali za
kuboresha sekta ya sekta ya Elimu.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inalo jukumu la kuhamasisha
uchangiaji maendeleo ya Elimu kote nchini ambapo, kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko
wa Elimu, Namba 8 ya mwaka 2001 sehemu ya 12 (1) (a) na (b) mchangiaji ni mtu
yeyote anayetoa mchango wa pesa, bidhaa, au huduma kupitia Mfuko wa Elimu wa
Taifa au kutekeleza mradi kwa uratibu wa Mfuko huo wa Elimu.
Aidha, mchangiaji anaweza kuwa mtu yeyote anayetoa udhamini au
ruzuku kwa wanafunzi mbali na watoto wake, familia yake au mwajiri wake, kwa
lengo la kuwasaidia kuendelea na elimu kwenye ngazi ya sekondari au elimu ya
juu ambapo udhamini huo atautoa kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.
Wadau na wachangiaji wa maendeleo ya Elimu kote nchini wanahimizwa
kutoa michango yao kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ili waweze kutangazwa na
kutambuliwa kitaifa, ambapo mchangiaji huandikwa
katika rejesta ya kudumu ya wachangiaji wa elimu,
Faida nyingine ya kuchangia kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ni kupata
Hati ya Utambuzi wa Uchangiaji wa Elimu (Certificate of Educational
Appreciation ambapo mchangiaji anaweza kuitumia kuomba nafuu ya kodi kutoka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mujibu wa Kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 marejeo ya
mwaka 2019.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni