Zinazobamba

RAIS DKT KIKWETE ASEMA BADO JITIHADA ZINAHITAJIKA TANZANIA KUWA NA ELIMU BORA

     Rais Msataafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Kikwete 

Na Mussa Augustine

Rais Msataafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Kikwete amesema kuwa bado kazi kubwa inahitajika.kufanyika kuhakikisha Tanzania inaboresha sekta ya elimu ili iendane na  kasi ya mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo yanategemea zaidi teknolojia.

Dkt.Kikwete amesema hayo Novemba 27,2023 wakati wa kongamano lililofanyika Katika ukumbi wa Serena Hoteli jijini Dar es salaam nakubainisha kuwa  licha ya serikali za awamu zote kuchukua hatua mbalimbali za kuleta mabadiliko kwenye sekta ya elimu lakini bado jitihada kuwa zinahitajika kuhakikisha Tanzania inafikia malendo katika Mapinduzi ya Viwanda.

Rais Dkt Kikwete amekabidhiwa tuzo na mtandao wa elimu Tanzania ( TENMET) iliyotambua mchango wake katika sekta ya elimu wakati wa utawala wake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano awamu ya nne.

Dkt.Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya Global Partner For Education(GPE) amesema hakuna awamu ya uongozi ambayo imemaliza kazi yote inayotakiwa kufanyika katika sekta ya elimu licha ya sifa nyingi kuelekezwa kwenye yongozi wake.

" Nilipewa jukumu la kujenga shule za kata ili wanafunzi waendelee na elimu ya sekondari hilo lilifanyika na baada ya miezi sita baada ya kutoka kwenye uongozi nilikutana na kijana mwenye umri wa miaka kumi na tano kule katikati ya Tabora na Nzega hajawahi kwenda shule ingawa anatamani kusima,sasa ukijiuliza kuna watoto wangapi hawajapelekwa shuleni" amesema Kikwete.

Aidha amesema kuwa baada ya Hayati Dkt. Pombe Magufuli kutekeleza mpango wa elimu bure,pia Rais Suluhu Hassan nae ameingia amefanya mengi ila bado kuna kazi kubwa inahitajika kuendelea kufanyika kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora kwa kuwa sasa tumejikita kwenye ubora tofauti wakati nimeingia madarakani kipaumbele ilikua ni upatikanaji wa elimu kwanza.

Ameongeza kuwa katika kipindi hiki ambacho mapinduzi ya nne ya viwanda yameshika hatamu tanzania inapaswa kuendana na maendeleo hayo kwa kuwa dunia haitatusubiri.

              Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dkt Chrles Msonde

Akizungumza wakati wa kufungua  kongamano hilo Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dkt Chrles Msonde ameaema kwamba mkutano huo umefanyika kwa muda muafaka ikizingatiwa Tanzania inafanya jitihada mbalimbali katika kuboresha elimu.

"Jitihada nyingi zimefanyika katika kuhakikisha tunakua na elimu bora ikiwemo kuongeza miundombinu,kuboresha ufundishaji ,mapitio ya sera na mitaala hayo yote yanalenga kuwa na elimu inayoendana na mahitaji ya dunia ya sasa"amesema Dkt Msonde

Nakuongeza kuwa " Kufanikisha yote haya ni lazima kuwepo ushirikiano wa kutosha kati ya serikali,sekta binafsi,wadau wa maendeleo na mashirika na yanayojihusisha na elimu kwa pamoja tuunganishe nguvu kuhakikisha tunakua na elimu bora" Amesema Dkt Msode.

Mratibu wa mtandao wa elimu Tanzania ( TENMET) Uchola Wayoga

Nae Mratibu wa mtandao wa elimu Tanzania ( TENMET) Uchola Wayoga amesema kufanyika kwa kongamano kunatoa fursa kwa wadau wa elimu ikiwepo serikali,watu wa sera ,vyuo vikuu wanafunzi ,walimu,watafiti, Taasisi za elimu,mashirika ya umma na binafsi na wadau mbalimbali wa elimu ndani na nje kujadili hali ya ubora wa elimu.

Wayoga amesema hatua hiyo inalenga kubadilisha mawazo na kushirikiana uzoefu kwa lengo la kuboresha utoaji wake nakuunda mustakabali bora wa utoaji wa elimu hapa nchini.

Wayoga amebainisha matarajio ya kongamano hilo nikutoa fursa na njia kwa watunga sera,watafiti,wasomi, wanafunzi,wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi kujadiliana na kushirikiana uzoefu wao na maarifa juu ya nafasi ya elimu katika kukabiliana na mabadiliko yanayokabili ulimwengu wa sasa

Kongamano hilo limeshirikisha washiriki kutika katika nchi zaidi ya kumi za afrika ambazo ni Tanzania,Kenya,Uganda,Ethiopia,Lesotho,Zimbabwe,Malawi,Msumbiji,Sudani kusini na Sudani kwa ajili ya kujadili hali ya ubora wa elimu katika nchizo.



Hakuna maoni