Zinazobamba




Na Mussa Augustine

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amezindua mwongozo wa kitaifa wa ulaji sahihi ulioandaliwa ili kuimarisha Matumizi sahihi ya chakula Mchanganyiko katika kutokomeza changamoto zote za utapiamlo hapa nchini.

Akizungumza leo Novemba 16, 2023 katika hafla ya uzinduzi huo Jijini Dar es Salaam Waziri Ummy amesema mwongozo huo umeandaliwa kwa kutumia taarifa na Takwimu za kisayansi zilizofanyika nchini na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 barani Afrika ambazo zinamuongozo kama huo.

“Nimefahamishwa kwamba mwongozo huu uliandaliwa kwa kuhusishwa Wadau mbalimbali kutoka ngazi zote. Pia wananchi wa kawaida walipata fursa ya kutoa maoni yao kwenye jumbe na michoro mbalimbali iliyotumika kwenye mwongozo huu,” amesema Waziri Ummy na kuongeza,

“Tunapozindua mwongozo huu, tunatekeleza moja kwa moja maelekezo ya Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kupanua wigo wa Utoaji taarifa za lishe kwa wananchi,”.

Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kuwashukuru Wadau wote walioshirikiana na Serikali katika kutokomeza utapiamlo wa aina zote.

“Leo kwa kipekee kabisa ninawashukuru FAO na Umoja wa Ulaya kwa mchango wao mkubwa katika kuunga mkono juhudi zetu za kuboresha hali ya lishe kwa Watanzania na kwa kufadhili maandalizi ya mwongozo huu. Asanteni sana FAO na Umoja wa Ulaya,” ameshukuru Waziri Ummy.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewaelekeza Maafisa Lishe, Wataalam wa Afya, Watafiti, Wataalam wanaotoa elimu ya lishe katika jamii, walimu na wadau wote wanaojishughulisha na Utoaji elimu ya afya ya jamii na lishe kuhakikisha wananchi wanafikiwa na kuutumia vizuri mwongozo huo.

Kadhalika ameielekeza Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) washirikiane na kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kuandaa jumbe fupi fupi zinazoweza kutumika katika vyombo mbalimbali vya habari kama vile Televisheni, Redio, Magazeti na Mitandao ya kijamii ili kufikisha ujumbe mahususi wa mwongozo huo.

Aidha Waziri Ummy amebainisha kuwa atawasiliana na OR Utumishi ili waelekeze Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa elimu ya lishe katika vikao vyote vinavyofanyika katika maeneo yao vinavyohusisha watu 50 au zaidi kama mkakati wa kurahisisha kukabiliana na uzito uliozidi na unene Serikalini.

Ametoa wito kwa viongozi hususan katika ngazi za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kuwa mwongozo huo unasambazwa na kutumika kikamilifu.

Hakuna maoni