Zinazobamba

TUNYISWA SISTERS: WAUGUZI WALIOIKOA TANZANIA (AWALI TANGANYIKA).


"Mheshimiwa afande, hawa ni wanandugu  nawapeleka Bechuanaland (sasa ni Botswana) kwenye mazishi ya ndugu yao na nitarejea nao baada ya mazishi." Yalikuwa maneno ya dereva wa basi ndogo ili kupata kibali cha kuvuka mpaka kutoka Afrika Kusini kuingia Bechuanaland (sasa Botswana). Dereva alikuwa mzungu, kijana wa Chuo kikuu cha Wits. Mpakani hapo alijitambulisha kama Padre ili kuaahadaa askari wa mpakani na pia hawakuwa na wasiwasi sana kwa kuwa alikuwa mzungu mwenzao. Lakini ulikuwa mpango uliofanywa na Mwalimu Julius Nyerere na Ally Skyes kupitia Oliver Thambo.


Kuinzungumzia kanuni ya Apartheid ni jambo kubwa katika historia ya Afrika Kusini. Apartheid neno la lugha ya Afrikaans likimaanisha "Apartness", yaani hali kutengana katika mambo mbalimbali. Mfano eneo fulani liwe la watu wa aina fulani tu na ni marufuku kwa mtu tofauti kukanyaga hapo, au upendeleo kwa watu fulani katika huduma na mambo mengine. Apartheid ilipewa nguvu na Sheria ya Group Area Act huko Afrika Kusini. Ndiyo maana mwanamuziki wa reggae wa Afrika Kusini, Luck Dube, kati ya nyimbo zake kuna wimbo unaitwa "Group Area", utafute usikilize anachokiimba. Apartheid ya kisasa huenda ipo hata hapa kwetu Tanzania. Macho ni yako, akili ni yako, fumbuka. Tuachane na hilo.


Hadithi ya watu hawa waliokuja kuikoa Tanzania huenda haijulikani na wengi hapa Tanzania lakini Afrika Kusini historia hii imetunzwa kwa ni ya kutuka sana. Hapa Tanzania mkoa wa Mbeya ni eneo la heshima Afrika Kusini sambamba na Morogoro. Achilia mbali Dar es Salaam ambayo wakati huo Ally Sykes walimuita "The Godfather of Dar Exiles."


Ndani ya TUNYISWA SISTERS wapo wenzao ambao si wa ukoo wa Tunyiswa lakini wanabebwa na title hiyo kutokana na mchango wao wakiongozwa na Edith Tunyiswa na ndugu yake Kholeka Tunyiswa. Ingawa kiongozi wa jumla alikuwa bwana  Ahmed Kathrana. Kwa nini waliletwa kuikoa Tanzania? Historia ya sekta ya Afya Tanzania inatupa jukumu la kuishukuru Afrika Kusini.


Mapema baada ya Uhuru wa Tanganyika, palitokea wimbi la ghafla tu kwa wauguzi wa Wazungu kujiuzulu wadhifa wao na kuomba kurudi kwao Uingereza. Walipoulizwa mboma wanafanya uamuzi wa ghafla hivi huku bado Tanganyika ikiwa na uhitaji mkubwa wa huduma yao? Walijibu kwamba hawako tayari kutanya kazi na Serikali inayoongozwa na mtu mweusi, Julius Kambarage Nyerere. Kwa hiyo no bora waache kazi na warudi kwao lakini si kuongozwa na mtu mweusi.


Lilikuwa pigo kubwa kwa sekta ya afya Tanganyika. Balozi Sindiro Mfenyanya anaeleza katika kitabu chake cha Walking with Giants: Life and Times of An ANC Veteran. Mwalimu Julius Nyerere aliongea na Ally Sykes wafanye nini ili kuokoa afya za Watanganyika walioachwa kwenye hospitali nchini ambapo idadi ya wauguzi imepungua ghafla. Wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika walikuwa na sababu muhimu kwao kumuitwa Ally Skye "The Godfather of Dar Exiles." Akili yake ya kipekee ingawa hatajwi sana.


Ally Aykes na Mwalimu Nyerere walikubaliana kwamba wakazungumze na Oliver Thambo. Wakati huo Oliver Thambo alikuwa uhamishoni mjini Dar es Salaam. Alipokelewa vema na aliishi vema na wenyeji wake. Na hapo alikuwa kiongozi wa chama cha ANC wakati wakipigania uhuru wa Afrika Kusini. Baada ya mazungumzo ya watu watatu hawa, Oliver Thambo alikubali kuchukua wauguzi wa Afrika Kusini waje kusaidia kutoa huduma Tanganyika. Ni wauguzi waliokuwa chini ya chama cha ANC. Waliwwkeza kwa muda mrefu kwenye maeneo mbalimbali ili kuwa na wataalamu.


Oliver alituma ujumbe haraka kwa wenzake Afrika Kusini. Kisha mpango ulianza kusukwa kwa umakini ili kutobainuka na Serikali ya kikoloni. Dar es Salaam, Mwalimu Nyerere na Ally Sykes walikuwa makini na jambo hilo kwa manufaa ya Watanganyika wote.


Wauguzi 20 waliandaliwa. Wakiwa bado wasichana wazuri kabisa walikubali kuweka rehani maisha yao wakati wa kusafiri kuja Tanganyika. Kwa vyovyote vile walijua kuwa kuvuka mipaka ya Afrika Kusini inaweza kuwa salama au si salama kwani serikali ya kikoloni ilikuwa makini kona nyingi za nchi hiyo. Basi ilibidi waandaliwe kimbinu kwanza hata kutumia vielelezo feki ili wasibaunike. Huku Tanganyika Mwalimu Nyerere na Ally Syskss waliamini Oliver Thambo hatakosea mpango wao waliousuka kwa manufaa ya Watanganyika wote.


Katika orodha yao waliwepo Edith Tunyiswa, Kholeka Tunyiswa, Nomava Ndamase, Eduth Ncwana, Mary Soconywa, Natalie Masimang na wengine. Balozi Lujobe Rankoe anakazia sifa kemkem waliozokuwa nazo wauguzi hawa walipokuja Tanganyika. Ni katika kitabu chake cha A Drem Fulfilled: Memoirs of An African Diplomat.


Wauguzi hao walitoka Afrika Kusini kwa basi ndogo na kupita mpaka wa Botswana. Dereva wa bas hilo alichukuliwa kijana mzungu wa Chuo kikuu cha Wits ambaye alikuwa amejipambanua kama Padre na hivyo kuwa rahisi kuvuka. Maakini ya Mungu askari wale mpakani hawakujua kuwa wameingizwa mjini na Mwalimu Nyerere na Ally Skyes kupitia Oliver Thambo.


Walifanikiwa kuvuka na kuendelea na safari hadi kwenye ngome ya chama cha ANC iliyokuwepo Botswana. Ni katika jumba la Kaitseng House eneo la Labatse. Hapakuwa na maiba wowote ma hivyo hawakwenda kwenye mazishi kama alivyoeleza dereva wakiwa mpakani. Hapo kilikuwa kituo chao cha kwanza tangu watoke Afrika Kusini.


Walipumzika hapo kwa muda wa mwezi mmoja wakiwa wanapata mafunzo ya ziada kuishi ugenini. Kwa sababu waliacha ndugu zao, wapendwa wao, mali zao ma mambo mengine kisha kukubali kuja Tanzania kuokoa afya za Watanganyika waliokuwa mahospitalini baada ya wauguzi wa kizungu kugoma na kutaka kuondoka, kisa hawakutaka kuongozwa na mtu mweusi.


Mwalimu Nyerere na Ally Skyes kupitia Oliver Thambo waliweka mkakati kwamba wawacheleweshe kidogo wauguzo hao ili kuwazuga maafisa wa serikali ya Afrika Kusini wakati huo. Basi baada ya mwezi mmoja waliokuwa nchini Botswana, ilikuja ndege maalumu kutoka Tanzania. Ndege ilikuja kwa kazi maalumu ya kuwachukua wauguzi hao. Safarik ikaanza. Hatimaye wauguzi wale walifanukiwa kuingia Tagantika na kupokelewa na baadhi ya Waafrika Kusini wenzao.


Ikawa hatua kubwa ya mafanikio makubwa ya Mwalimu Nyerere na Ally Skyes katika sekta afya ungawa idadi ilikuwa ndogo lakini walikuja kutumia mbinu nzuri ya kwamba wauguzi hao wakiwa wanafanya kazi yao, pia watumike kutoa mafunzo Watanganyika wengine waliojiunga na fani hiyo.


Kholeka Tunyiswa alipelekwa Tanga. Baada ya kufanya kazi lwa muda huko Tanga, alihamishiwa Iringa. Baadae alipelekwa hospitali ya Mwananyamala iliyopo Dar es Salaam. Pia, alifanya kazi hospitali ya Mnazi Mmoja na Magomeni zilizoko Dar es Salaam.


Edith Tunyiswa alipangwa Mbeya. Huko Mbeya sifa zake zikawa za kutukuka sana. Alifanya kazi kwa ziada ya pale alipotakiwa kuishia. Alitumia pia mshahara wake kusaidia watu waliokuwa na shida mbalimbali. Aliwasaidia chakula na malazi Waafrika Kusini walioingia nchini kuomba hifadhi Dar es Salaam kupitia Mbeya. Sifa zake ziliwavutia wengi. Kijana mmoja wa Tanzania alijitosa na kumposa Edith kisha walifunga ndoa hapa hapa Tanzania. Vilevile Kholeka Tunyiswa aliolewa Dar es Salaam.


Ndugu wawili hawa Kholeka Tunyiswa na Edith Tunyiswa wanabeba wenzao wote waliokuja nao. Wote walifanya kazi kwa bidii na kwa ustadi mkubwa. Inaelezwa kwamba Kholeka Tunyiswa alikuwa anapenda wageni nyumbani kwake Magomeni. Hivyo alikuwa na kawaida ya kupika maandazi mengi ma chapati nyingi. Akija mgeni, anapewa ale kadiri awezavyo.


Zoezi hili lililoandaliwa na Mwalimu Nyerere na Ally Skyes kupitia Oliver Thambo lilisaidia kupata wauguzi wengine wengi walipfumdishwa na timu hii ya wauguzi 20 kutoka Afrika Kusini. Kati yao wapo waliobaki Tanzania, mfano Kholeka Tunyiswa alibaki na amwfariki mwezi March 2023, Dar es Salaam.


Ndiyo sekta iliyookolewa na wauguzi hawa 20 kutoka Afrika Kusini kama alivyoweka kumbukumbu zake Balozi Sindiro Mfenyana kwenye kitabu chake nilichotaja aya za mwanzo, kadhalika Balozi Lujobe Rankoe. Urafiki wa Tanzania na Afrika Kusini uko namna hiyo. Wauguzi hawa kati yao wengine walienda kuongeza maarifa Urusi na kurejea kufanya kazi kwenye kambi za chama cha ANC.


Kholeka Tunyiswa alifariki tarehe 5 March 2023 na alifanyiwa ibada ya kifamilia nyumbani kwake Dar es Salaam. Lakini mwili wake baada ya muda mfupi ulisafirishwa hadi Kijijini alikozaliwa na kuzikwa kwa heshima zaidi. Yeye alipata mafunzo ya uuguzi na masuala ya kupigania uhuru chini ya mkufunzi wake Govan Mbeki, huko Eastern Cape, Afrika Kusini. Ndugu yake Edith Tunyiswa alifariki mwaka 2021, aliongeza jina Pemba na kuwa Edith Tunyishwa Pemba kwa heshima ya mume wake Mtanzania.


Chama cha ANC kilikuwa na makada wake wa kufumdisha Vijana katika maeneo mbalimbali. Albertina Susulu alikuwa kada wa mkoa wa Transvaal, John Makathini alikuwa Kwa Zulu Natal, na Govan Mbeki alikuwa Eastern Cape.


Pichani ni Kholeka Tunyiswa wakati wa uhai wake, na picha ya tangazo la ujio wa mabaki ya mwili wake na Afrika Kusini.


Mungu awape pumziko la milele wauguzi hawa waliotangulia kwake. Vilevile kwa waliofanya mpango huu hadi kufanikiwa.


Wasalaam,

Kizito Mpangala 

September 2023.

Hakuna maoni