Zinazobamba

Tumekwama wapi Ithibati ya bidhaa halali?



 

Binafsi napenda sana nyama, kama wanavyopenda Watanzania na Waafrika au hata labda wanadamu wote, ukiacha wale waliojiharamishia.

Hata hivyo, ulaji wangu wa nyama umepungua sana, hasa nje ya nyumbani. Hii ni kwa sababu ya kujiwekea masharti mengi kwa sababu ya mashaka ya uhalali na usalama wa nyama zinazouzwa. Kwa mfano, sili kuku kwenye sehemu za wauza chipsi na baadhi ya migahawa. Mashaka yangu si ya bure.

Upo ushahidi kuwa watu wengi siyo waaminifu katika mnyororo mzima wa biashara ya nyama kuanzia wanakotolewa hadi kwa wauzaji wanaopeleka bidhaa hiyo kwa mlaji (sehemu wanazouza vyakula). Kwenye nguzo zote nne za uchinjaji halali yaani mnyama, vifaa, mchinjaji na taratibu za uchinjaji, kuna ukakasi na wasiwasi mkubwa.

Kinachonipa mashaka zaidi ni ushahidi mbalimbali niliopata kuuona na kuusikia kuhusu nyama tunazokula.

Mara kadhaa kwenye mitandao ya kijamii tumeona video za wanawake wakiwanyonga kuku kwa mikono badala ya kuwachinja. Wengine wanachinjwa kwa ukatili wa hali ya juu kwa visu butu, kisha wanaachwa wanapaparika.

Juzijuzi tu nilisikia tena huko Bagamoyo, maeneo ya Mapinga, Kerege na Kiaraka, ambako kuna ufugaji mkubwa wa kuku kuwa kuna utaratibu wa kukusanya vibudu na kuwauzia wanawake.

Wanawake hao, kila asubuhi kati ya saa 1 na 3 au jioni kuanzia saa 12 hadi mbili usiku wamekuwa wakionekana wakienda na kurejea na ndoo zilizojaa nyamafu (vitoweo mfu).

Rafiki yangu mmoja aishiye Kibaha aliwahi kunihadithia kuhusu ng’ombe wanaofia njiani (kutoka huko wanakotolewa) na kushushwa Kibaha kisha huchinjwa na kuingizwa sokoni. Siku moja alipoenda buchani, rafiki yake muuza nyama akamwambia leo usinunue hii ni kibudu. Mara ngapi tunasikia watu wamekamatwa kwa kuuza mishkaki ya nyama za wanyama wasioliwa kama mbwa na kadhalika?

Katika mazingira haya, siyo tu tupo hatarini kula haramu, lakini pia afya zetu pia ziko matatani kwa kula vitu vibaya, kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu aliyesema: “Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za Shetani. Hakika yeye ni adui yenu aliye dhaahiri.” [Qur’an, 2:168]. Vilivyo halali bila shaka ndiyo vizuri pia.

Haihitaji sayansi ya roketi kujua kuwa viwango vya halali vya Uislamu siyo tu suala la kiimani bali vinamhakikishia mwanadamu usalama wake anapotumia bidhaa husika.

Imethibitika kisayansi mnyama asiyefaa kuliwa, au yule anayefaa lakini mgonjwa au amechinjwa isivyotakiwa, anaweza kumsababishia mwanadamu madhara na maradhi mbalimbali.

 

 

Ziko wapi bidhaa halali?

 

Katika mazingira haya, tunajiuliza ziko wapi bidhaa za halali ili tuweze kula vizuri kama Uislamu unavyotutaka? Jitihada kadhaa zimefanyika katika kuanzisha kampuni za kutoa ithibati ya halali kuthibitisha ubora wa huduma na bidhaa, ikiwemo nyama. Sasa hivi kuna kampuni ya MICO International Halal Bureau (MIHB) ikibeba jukumu hilo na kutoa cheti.



Hata hivyo, licha ya uwepo wa kampuni hiyo, kuna changamoto nyingi bado ikiwemo mwamko mdogo wa jamii unaopelekea uwepo wa watoa huduma wachache waliothibitishwa. Na hata hao waliothibitishwa, hawajulikani kwa walaji wengi wa kawaida.

Tathmini yangu ni kutoka katika mtazamo wa mlaji. Naishi Mburahati lakini silijui duka lolote ambalo lina ithibati ya halali siyo tu Mburahati bali pia maeneo ya jirani kama Manzese, Kigogo, Mabibo na hata Magomeni. Sisemi hayapo bali siyajui kwa sababu taarifa hazifiki kwangu na nikizitafuta sizipati. Huu ni udhaifu mkubwa katika maendeleo ya kuweka ithibati ya halali ya bidhaa siyo tu nyama bali zote na huduma pia.

Ofisa mmoja wa MICO aliniambia kuna shida pia kwa watoa huduma kutokuwa tayari kugharamia zoezi la kufanyiwa ithibati. Hii ni sahihi lakini labda kampuni yenyewe ingejitahidi kuwepesisha gharama kwa kutafuta wafadhili.

Ithibati ya halali ni jambo la kiibada na isingefaa lifanyike kwa madhumuni ya kibiashara zaidi. Tukishindwa kuweka na kuvisimamia hivi viwango, tumeshindwa wote kama umma na madhara yanarudi kwa jamii nzima.

Natoa rai kwa kampuni kubwa za Waislamu ziingie kwenye biashara ya bidhaa halali, hususan bidhaa za nyama ili Waislamu na jamii kwa ujumla tununue na kula nyama kwa kujiamini.

Watu wangu wa nyumbani wanapenda sana soseji lakini kama hatujui zinatoka wapi na zinatengenezwaje, na kama je, viwango vya halali vimefikiwa au la, ni ngumu kununua tu na kula ovyo.

Masheikh nao tunawapa rai wajitahidi kuzungumzia umuhimu wa kutumia bidhaa na huduma halali ili kuongeza uelewa na mwamko wa Waislamu. Uimara wa ithibati ya halali utapatikana tu kama kuna watumiaji wa kutosha.

 

 

Tujifunze kwa wengine

 

Waislamu wa Tanzania tunaishi kwa mazoea sana. Wenzetu katika mataifa mengine wanachukulia masuala haya kwa umakini mkubwa na ndiyo maana kumekuwa na vikwazo katika upelekaji bidhaa, hususan za nyama, katika nchi za Kiislamu.

Ajabu ni kuwa sisi wenyewe, licha ya ushahidi mwingi wa kukosekana uadilifu katika mnyororo mzima wa thamani katika uandaaji bidhaa za nyama, bado tunadhani bidhaa tunayoikuta buchani, hotelini, migahawani ni safi na imekidhi vigezo huku tukijificha kwenye kigezo kuwa kwa kuwa hatujui, haina tatizo.

Binafsi, hatari ninayoiona katika bidhaa za nyama Tanzania naifananisha na hali ya China, ambako niliishi kwa mwaka mmoja. Kule mara mbili nilikula nguruwe, bila kujua.

Siku nilipofika katika mgahawa wa chuo, nikaagiza wali na samaki lakini kumbe waliweka nyama ya kusaga ya nguruwe. Siku nyingine nikatoka na rafiki aliyekuwa akinifundisha kichina nikaagiza tambi na yai. Nilipoanza kula, nilipozamisha vile vijiti vyao (chopstick) kwenye bakuli nikaibua pande la nyama.

Mazingira tofauti lakini hatari ni ileile. Jiulize mwenzangu unayejisosomola makuku kwenye vibanda vya chipsi, mara ngapi umekula wale kuku vibudu au nyama kibudu aliyefia njiani na kushushwa pale Kibaha au wale waliochinjwa baada ya kuuawa kwa kwa maji ya moto, wanaofugwa kwenye vitongoji mbalimbali vya hapa Dar es Salaam?

Tuchukue tahadhari kama umma kwa kuunga mkono ithibati ya bidhaa za halali.

 


 


Hakuna maoni