Zinazobamba

Ni bora Mtaala wa EDK uwe chini ya BAKWATA-wadau

 


Ni bora Mtaala wa EDK uwe chini ya BAKWATA-wadau

Na Mwandishi wetu,Dodoma

Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislam wameiomba serikali iwe makini na suala la mtaala wa somo la dini ya Kiislam, wengine wakienda mbali wakisema ni kheri mtaala huo uwe chini ya Bakwata kuliko ilivyo sasa

Abbdallah Sued, kutoka Dodoma amesema sababu kubwa za yeye kupendekeza mtaala huo kuwa chini ya Bakwata ni kutokana na ukweli kuwa hivi sasa mtaala huo umehodhiwa na kundi  moja, na kwamba waislam wengi wanalalamika kutoshirikishwa

“Mimi ningeweza ningemwambia Wazir Prof Adolph Mkenda awe makini katika hili, akitoa mwanya wa kuamini kikundi flani na kuacha mapendekezo ya waislam wengi italeta shida huko mbeleni

“Ukiona watu wanatumia nguvu kubwa katika hili kuna maslahi yanapiganiwa, ni bora baraza la Bakwata lipewe jukumu hili, tutafurahi sana,” aliongeza

Naye, Mwadini Ali, akizungumza na mtandao huu alikosoa baadhi ya harakati zinazofanywa na waislam wanaopigania mtaala wa EDK, akisisitiza kuwa wengi wamekuwa wakitanguliza maslahi.

“Nimesikia tamko la Baraza kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislam likisema serikali inafanya hadaa katika mchakato huu, shida yangu ni kwamba hadaa hiyo ni kwa maslahi ya nani?, alisema

Aidha, akieleza ukosefu wa weledi wa baadhi ya wanaharakati wa mtaala, Ali, amesema viongozi walio mbele wanaheshimika katika jamii kutokana na mchango wao katika kufanikisha mambo mengi ya waislam lakini kasi wanayoenda nayo sasa inafikilisha.

Hivi karibuni, Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania limeelezea kusikitishwa kwake kwa serikali kuendelea kuiweka rasimu ya somo la dini ya kiislam (EDK) katika tovuti ya TET na kuongeza kuwa jambo hilo linawatatiza kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza na vyombo vya habari Septemba 27, 2023 Jijini Dar es Salaam, Amir wa Jumuiya hiyo Alhaj Sheikh Mussa Kundecha amesema uwepo wa rasimu hiyo katika tovuti ni ishara kuwa serikali bado haijakubali mapendekezo ya vikao na kwamba huenda ni hadaa kwa waislam

Sheikh Kundecha ambaye alifika kwenye kikao hicho kwa lengo la kutoa mrejesho wa vikao mfululizo vilivyofanyika, amesema kinachowatia wasiwasi Zaidi ni kuona licha ya jitihada zote zinazofanyika lakini bado kuna watendaji wanaonesha wazi kutokuwa tayari na makubaliano ya vikao

“Hadi sasa ukitembelea tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania kwenye kiunga cha ‘mitaala, mihtasari & moduli’ ipo mihtasari ya masomo 15 yanayofundishwa kwa sasa, masomo ya dini mihtasari yake haikuwekwa kwa kuwa TET haina haki miliki ya mtaala wa dini.

 Lakini cha ajabu katika kiunga cha ‘machapisho’ (rasimu ya mitaala mipya na mihtasari ya elimu ya sekondari- ipo mihtasari ya masomo 27 likiwemo somo la elimu ya dini ya kiislamu ambayo inaeleza hati miliki yote ni ya serikali hadi kudurufu ni kosa kisheria bila kupata idhini ya maandishi,” alisema Sheikh Kundecha.

 Alisema katika kikao chao na Waziri wa elimu kilichofanyika Agosti 12, 2023, walikubaliana suala la umiliki wa mtaala libaki kwa Waislamu wenyewe na kwamba michakato yote iliyokuwa ikiendelea na TET ilipaswa kusimama

Pia katika kikao cha Agosti 29, 2023 katika Ukumbi wa Mohammed VI uliopo Kinondoni, waislam kwa umoja wao waliazimia suala la mitaaya ya EDK linabaki kwa waislam wenyewe.

Aidha, alisema wanachojiuliza ni kwamba ni msukumo upi wa upendo na wema unaopelekea kuvunja katiba ya nchi, kukiuka walichokubaliana kwenye vikao kwa kuendelea kuweka rasimu hizo katika tovuti na kwamba kwa nini wasiamini kuna nia ovu ya kupotosha mafundisho ya dini.

 Vilevile Baraza hilo limeisihi serikali kuepuka hujuma na uvujifu wa katiba unaofanywa na baadhi ya watendaji wachache wanaotaka kutumia vibaya nafasi zao, kuchafua hali ya amani na utulivu ama kwa msukumo wa makabila, Imani na ukanda.

Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda tayari imesema ipo tayari kusikiliza na kupokea maelekezo yeyote kutoka kwa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir juu ya namna nzuri ya usimamizi wa somo la dini ya kiislam.

Prof Mkenda alitoa kauli hiyo Agost 29, 2023 katika mkutano wake na viongozi wa dini ya Kiislam uliofanyika katika ukumbi wa Mohammed VI Kinondoni Jijini Dar es salaam.

Pia, Prof aliwatoa watu hofu huku akisema ofisi yake bado haijafunga milango ya kupokea maoni na ingawaje sikio lake limebaki kwa ofisi ya Mufti ambayo ndicho chombo kikuu cha umma wa kiislam.

Prof Mkenda amewahakikishia umma wa kiislam kuwa haitaingilia matakwa ya waislam katika somo hilo na kwamba maoni yatakayotolewa na ofisi ya Mufti yatachukuliwa kwa uzito mkubwa kwani ndiyo yanayobeba matakwa ya waislam hapa nchini.

Aliwahakikishia waislam kuwa maudhui ya mitaala yatawekwa na masheikh, waumini na wanazuoni wenyewe huku akisisitiza hakuna shaka itakayokuwa na afya ikiwa katika masuala ya dini isipokuwa katika maeneo mengine.

Jitihada za Barza.I.E.P

Akieleza Jitihada ambazo zimefanywa na Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Sheikh Kundecha amesema tayari wamekamilisha mchakato wa uandaaji wa muhutasari wa Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa Sekondari ambapo Septemba 22, 2023 tayari wameukabidhai TET kwa ajili ya hatua zinazoendelea.

Pia, amesema kazi ambayo inaendelea kwa sasa ni maandalizi ya kitabu cha kidato cha kwanza ambapo amesema inshaallah kitakuwa tayari kutumika ifikapo Januari 2024 kama alivyoshauri Mkurugenzi wa TET katika kikao cha Agosti 12, 2023.

 


Hakuna maoni