Zinazobamba

Tamko la TEC kuhusu uwekezaji katika bandari ya Dsm lakosolewa kila kona

 




Na Mwandishi wetu, Fullhabariblog

Siku chache baada ya Baraza Kuu la Maaskofu wa Kikatoriki (TEC) kutoa Tamko lao kuhusu suala la bandari, watu wengi wamekosoa tamko hilo wakisema limejaa udini na wengine wakienda mbali kabisa wakisema aliyewasilisha ameongeza maneno yake.

 

Mbali na kuongeza maneno katika waraka, pia wadau wanasema Kitima hakuwa uhalali wa kuwasilisha tamko zito kama hilo kwani tayari alishaonyesha kuchagua upande.

 

Mmoja wa wadau waliokosoa tamko hilo ni Shemasi George Rugambwa kutoka Seminari ya Ntungamo, Bukoba, ambaye ametoa waraka maalum wenye maswali sita akihoji uharaka wa TEC kuleta andiko ambalo lina mapungufu mengi

Shemasi Rugambwa anasema anaamini ufafanuzi wa Padri Kitima kuhusu tamko la TEC unaweza kuwa na maneno yake binafsi ya ziada kwani alijipambanua awali kuwa na maslahi na jambo lenyewe.

 

Maswali sita anayohoji Shemasi Rugambwa…

Katika andiko lake, Shemasi huyo kutoka Bukoba, amehoji mambo sita ya msingi, ambayo mpaka sasa walengwa wameshindwa kujibu hoja na kubaki kulalamika kuwa aliyetoa andiko siyo Shemasi. Maswali yenyewe haya hapa

 

1. TEC inafahamu kwamba mwaka 1992 wakati Serikali inapitisha mfumo wa vyama vingi ulikuwa umekataliwa na asilimia 77 ya Watanzania? Hata hivyo serikali ikaamua uruhusiwe. Hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.

2. TEC inafahamu kwamba mwaka 2001 baada ya matokeo ya Uchaguzi wa Zanzibar na mauaji ya wafuasi wa CUF mwezi Januari, asilimia kubwa ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla walitaka kuwepo na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na SMZ na SMT chini ya Mkapa haikutaka? Hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.

3. TEC inafahamu kwamba mwaka 2014 maaskofu wote Katoliki Tanzania akiwemo Kardinali Pengo na wasaidizi wake walipokea mamilioni ya shilingi pesa taslimu na nyingine kwenye akaunti zao kama Askofu Nzigilwa (milioni 80 benki) na Kilaini (milioni 40 benki). Inajua fedha hizo zilitoka katika kampuni yenye makando kando ya rushwa ya kihistoria Tanzania. Wananchi wengi walipiga kelele lakini fedha hizo hazikurudi wala hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.

4. Padri Kitima anasema kwa zaidi ya miaka 60 ama toka tupate uhuru bandari yetu haijawahi kuendeshwa na wageni. Hii ni kauli yake au ya maaskofu wa TEC? Ni kweli TEC haifahamu kwamba kwa zaidi ya miaka 22 Bandari yetu ya Dar imekuwa chini ya kampuni ya TICTS ikiendeshwa kwa ubia na kampuni toka Hong Kong (Hutchsons?). Kama wanafahamu, wanakumbuka wabia wazawa wa kampuni hiyo wanahusika kwenye kuwapa hela maaskofu kama Rugemalira na IPTL yake walivyofanya? Hili wamewahi kuwaambia waumini wao katika mimbari za ibada?

5. TEC wanafahamu kwamba mwaka 1998 kwenye mauaji pale Mwembechai walikufa wasio na hatia na ilikuwa rai ya mamilioni ya Watanzania kutaka kuwepo na suluhu ya kisiasa? Hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.

6. Padri Kitima anasema wananchi wamelikataa Bunge? Ametumia kipimo gani cha Kikatiba? Maana wananchi wanalikataa Bunge kwa kutowachagua Wabunge kwenye Uchaguzi. Hii “Vox Populi Vox Dei” ya TEC imetumia kigezo gani? Wananchi wakikataa Bunge pia si wameikataa Serikali? TEC inaomba vipi busara ya Mheshimiwa Rais ambaye wakati huo huo inasema serikali yake imekataliwa? Kuna kuchanganyikiwa na haraka kubwa kwenye tamko la TEC hata namna lilivyochapwa na kupangiliwa. Inanipa mashaka kwamba chombo hiki muhimu cha Kanisa kimekubali kutumika kwa maslahi binafsi bila tafakari ya kutosha.

Je hii “Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu” ni wengi wapi hasa? Na mungu anayetajwa hapa ni nani? Usikute mungu anayetajwa na kusemwa asikilizwe ni mungu au miungu watu waliokuwa wanaingiza miamala kwenye akaunti za baadhi ya maaskofu wetu na viongozi wengine wa dini miaka nenda rudi. Tujihadhari. Tusiigawa nchi kupitia madhabahu,”  Alimaliza


Hakuna maoni