Zinazobamba

Na Mussa Augustine.

BENKI ya Maendeleo imesema kwa mwaka 2022 imesajili ukuaji wa faida wa asilimia 184 na asilimia 163 mwaka kwa mwaka wa faida kabla na faida baada ya kodi mtawalia na kuwezesha kupata faida ya kwa wanahisa ya asilimia nane, na mapato kwa kila hisa ya shilingi za kitanzania 50.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 30, 2023 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank Plc Dkt. Ibrahim Mwangalaba amesema kwamba faida ya Benki kabla ya kodi iliongezeka hadi shilingi za kitanzania bilioni 2.02 kutoka shilingi za kitanzania milioni 710 mwaka 2021 wakati faida baada ya kodi iliongezeka kutoka shilingi za kitanzania milioni 587 hadi shilingi za kitanzania bilioni 1.3122 mwaka 2021.

Dkt. Ibrahim Mwangalaba ameleza kuwa ukuaji wa kuvutia wa faida ulichangiwa zaidi na timu iliyojitolea na kuangalia mbele kuona benki kuwa moja ya wadau muhimu wa sekta katika ukuaji wa uchumi.

“Ningependa kuangazia baadhi ya vichochezi, vya faida ambavyo ni pamoja na, ukuaji wa jumla wa mapato kwa asilimia 22 mwaka hadi mwaka kutoka shilingi za kitanzania bilioni 12.8 hadi shilingi za kitanzania bilioni 15.6 mwaka 2022,” amesema na kuongeza,

“Mapato halisi yaliongezeka kwa asilimia 31 kutoka shilingi za kitanzania bilioni 7.6 mwaka 2021 hadi shilingi za kitanzania bilioni 9.9 mwaka 2022. Biashara ya mikopo kutokana na kuimarika kwa hali ya uchumi, tumeboresha ubora wa vitabu vya mkopo kutoka mikopo chechefu asilimia 12 mwaka wa 2021 hadi asilimia 5.2 mwaka wa 2022, hii imechangia pakubwa mapato mazuri katika mwaka huu,”.

Amesema kuwa amana za wateja ziliongezeka kwa asilimia 11 kutoka shilingi za kitanzania bilioni 70 mwaka 2021 hadi shilingi za kitanzania bilioni 77 mwaka 2022 wakati mikopo na malipo ya awali kwa wateja yaliongezeka kwa asilimia 5 kutoka shilingi za kitanzania bilioni 57 hadi shilingi za kitanzania bilioni 60 mwaka 2022.

Dkt. Mwangalaba amesema mikakati iliyotumika katika uhamasishaji wa amana za wateja ilichangiwa zaidi na kuongeza thamani ya bidhaa na huduma ambazo benki imekuwa ikitoa.

“Kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za benki kupitia bidhaa za kidijitali kama vile huduma za kibenki kwa njia ya simu, mawakala wa Maendeleo Bank wanaofikia 1,200 waliopo zaidi ya mikoa 11 zimechangia ukuaji ulioonekana,” ameeleza Dkt. Mwangalaba na kuongeza kwamba,

“Benki ina mtaji wa kutosha katika hadhi yake na sasa tunatazamia kufanya kazi nchini kote punde tu tutakapolidhi mahitaji ya mtaji wa udhibiti kwa hadhi ya benki ya kitaifa,”.

Kwamba ingawa mtiririko wao wa mapato unatoa picha ya kuvutia, hata hivyo bado wako makini kuhusu menendo wa uchumi wa dunia  na wamekuwa wakifuatilia ipasavyo katika mwaka uliopita.

Amebainisha kuwa maendeleo Banki imekuwa na utendaji mzuri wa kifedha kwa mwaka 2022, ikijenga msingi thabiti wa utendaji kazi kwa mwaka 2023 wanapopanga kupanua kwa kufungua angalau tawi moja na mawakala wapya zaidi ya 500.

Amesema Benki inawekeza kwenye teknolojia kwa kutambulisha thamani ya bidhaa za kidijitali kama benki ya mtandao (internet banking), mfumo wa ukusanyaji wa malipo (PCS), GepG, mkopo kwa simu.

“Hii itawezesha benki kuongeza faida kwa fedha za wanahisa kufikia zaidi ya asilimia 10 kwa mwaka 2023 na kuboresha njia mbadala kwa wateja wetu. Ujumuisho wa kifedha kupitia utangulizi wa bidhaa mpya za kibunifu kama vile vijana na wanawake zitakuwa lengo letu kwa mwaka 2023,” amesema Mkurugenzi huyo wa Benki ya Maendeleo Plc.

Hakuna maoni