KC Mabwepande yawaunganisha wananchi na viongozi wao kujadili changamoto za kata hiyo kwa pamoja
Picha ya Viongozi wa Serikali za Mitaa mbalimbali na Kata Mabwepande wakiwa katika picha ya Pamoja baada ya Mdahalo. |
Na Vicent Macha DSM.
Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Mabwepande Kimewakutanisha wananchi, Pamoja na viongozi mbalimbali wa Mitaa na Kata ya Mabwepande, lengo likiwa ni kutoa mrejesho wa changamoto walizoziibua na namna ya kuzitafutia ufumbuzi baada ya kupewa elimu hiyo na TGNP mwezi Machi mwaka jana.
Akiwasilisha
changamoto hizo kwa viongozi hao Mwenyekiti wa Kituo hicho Bi. Fatuma Ramadhani
Nurru amesema kuwa Kata hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya Maji Safi na
salama kwa baadhi ya maeneo, Barabara, Elimu, Masoko ya kufanyia Biashara Pamoja
na Ukatili wa kijinsia.
Akiongelea changamoto
ya Ukatili wa Kijinsia amesema kuwa wao kama Kituo wamekuwa wakipokea kesi
mbalimbali za wanawake kupigwa na wanaume zao, lakini pia Watoto kufanyiana
vitendo vya ubakaji na kulawitiana wenyewe kwa wenyewe.
Ameongeza
kuwa kumekuwa na baadhi ya changamoto kwenye kufikia Elimu kwani kwa upande wa
Bunju “B” hakuna Shule ya Msingi hivyo inawalazimu Watoto kuvuka Barabara kuu
ya Bagamoyo na kwenda upande wa pili kufuata shule hali inayochangia Watoto kugongwa
na magari mara kwa mara.
Na mwisho
amewataka viongozi na wananchi kuweza kushirikiana ili kuleta maendeleo katika
kata hiyo kwani maendeleo hayawezi kuletwa na viongozi peke yake bali ni kwa
ushirikano wa makundi yote mawili wananchi na viongozi wao.
Mdahalo Ukiondelea. |
Kwa upande wake
Diwani wa Kata hiyo Mh. Muhajirina Kasimu Obama amesema kuwa kwa upande wa Mabwepande
wako vizuri kwani mahitaji mengi ya msingi wanayo, akizungumzia upatikanaji wa Maji
amesema kuwa huduma hiyo imeweza kufika katika Mitaa yote minne na kwasasa zoezi
hilo lipo katika Mtaa wa Mbopo na linakwenda vizuri kabisa.
Ameongeza kuwa
kwa upande wa Elimu pia wako vizuri kwani kata zote Nne zimebahatika kupata Shule
za msingi na sekondari, na kutoa ufafanuzi kuwa kwa changamoto ya Watoto wa Bunju
“B” Serikali inalitambua hilo hivyo muda si mrefu wataweza kupata Shule na
kuondokana na hadha ya kuvuka barabara kubwa ya Bagamoyo kufuata masomo.
Diwani huyo ameendelea kusisitiza kuwa Kata ya Mabwepande ni kata kubwa sana hivyo wanafunzi ulazimika kutembea kilometa 2 mpaka 5 kufuata masomo hivyo wao wakabuni mbinu nzuri ya kuhakikisha Watoto watakaomaliza elimu ya msingi katika shule moja wanahakikisha wanampanga katika shule ya karibu na Mtaa wake ili kupunguza umbali mrefu wa kufuata shule ilipo.
Aidha Diwani
huyo amemaliza kwa kusema kuwa changamoto ya barabara ameshaiwasilisha
Halmashauri na inaendelea kufanyiwa kazi kwani barabara nyingi za kata hiyo ni za Changarawe
na hazijafanyiwa marekebisho kwa muda mrefu hali inyofanya kutopitika kwa
urahisi hali inayosababisha kukosekana kwa Daladala zenye ruti ya Mabwepande,
na kuongeza kuwa changamoto hiyo inawafanya wakazi na wanafunzi kuzunguka sana wakati
kuna njia nyepesi ambayo ingeunganishwa na daladala.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika kazi za vikundi. |
Nae Mwenyekiti
wa Mtaa wa Mji mpya Mohamed Bafta amesema kuwa kilio cha Wananchi kilikuwa ni
soko hivyo serikali ikaamua kuwajengea soko changamoto iliyokuja kutokea wafanyabiashara
wengi wamejenga vibanda na badala yake hawavitumii hali iliyofanya kudhoofika
kwa soko hilo, na matokeo yake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni ametoa
maagizo ya kuwa wote wasiyovitumia vibanda hivyo waviondoe mara moja.
Kwa upande wake Mtafiti wa Elimu Wilaya ya Kinondoni ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu Kata ya Mabwepande Dkt. Bill Abraham amsemea kuwa sababu kubwa inayosababisha elimu kushuka katika kata hiyo ni kwamba walimu wengi wanaokuja katika kata hiyo wanakuwa wamekuja kutumikia adhabu na siyo kutekeleza wajibu wao.
Akitoa
ufafanuzi huo amesema kuwa walimu wamekuwa wakiambiwa na wakubwa wao wa kazi
kwa kuwa umefanya kosa hili adhabu yako nakupeleka Mabwepande hivyo na wao wanaona
ni kama sehemu ya kutekeleza adhabu kutoka kwa wakubwa wa kazi na siyo kutoa
elimu bora.
Ameongeza kuwa
wakazi wa kata hiyo pia hawakuipa elimu kipaumbele kwani linapokuja suala muhimu
la shule wazazi ulipuuzia kwa mfano kuhusu suala la masomo ya ziada kwa
wanafunzi au suala la chakula hivyo husababisha Watoto kusinzia Darasani na
kutofanya vizuri katika masomo yao.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni