TANROADS yaelekezwa kukata malipo kwa wakandarasi wazembe
KATIBU Mkuu wa Chama Chama Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo amechukizwa na ucheleweshwaji wa ujenzi wa barabara hivyo ameitaka Wakala wa Barabara Nchini(Tanroads) kuanza kuwakata fedha wakandarasi wanaochelewesha kukamilisha ujenzi wa barabara za mikoa kama zilivyoainishwa kwenye mikataba ya ujenzi,ili iwe fundisho kwa wengine.
Agizo hilo amelitoa jana katika Kata ya Mwaniko Kijiji cha Vuchama wakati akikagua ujenzi wa Barabara ya Mwanga- Kikweni- Vuchama inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 28.9.
Akikagua barabara hiyo inayojengwa na wakandarasi tofauti akiwemo M.S/Builders Limes works, Chongolo alisikitishwa na kasi ndogo ya mkandarasi anayejenga sehemu ya kipande cha barabara hiyo ambapo ujenzi wake unapaswa kukamilika Agosti 8, mwaka huu.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa ujenzi huo Meneja Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro Motta Kyando alisema barabara hiyo ni ya hadhi ya mkoa na ina urefu wa km 28.9 na kati ya hizo km 14.62 zinajengwa kwa kiwango cha lami na km 14.36 zinajengwa kwa kiwango cha changarawe.
Alisema utekelezaji wa ujenzi unaendelea lakini mkandarasi anajenga kwa kusuasua na kutoa sababu mbalimbali kama uwepo wa mvua na kusema walimuongezea muda hadi Agosti 8,mwaka huu ujenzi uwe umekamilika.
"Mkandarasi alitoa sababu kwa mradi kutokamilika awali na tukamuomgezea muda hadi Agosti 8,mwaka huu na baada ya hapo tutaanza kumkata fedha asilimia kwa sababu amekiuka makubaliano ya mkataba wa ujenzi,"alisema Kyando.
Akizungumzia ujenzi huo Chongolo alisikitishwa na mradi kuchelewa kukamilika na kuitaka Tanroads ifikapo Agosti 8,kama mkandarasi atakuwa bado hajakamikisha,waanze kumkata asilimia ya fedha ili iwe fundisho kwa wengine.
"Ifikapo Agosti 8,siku ambayo anatakiwa kazi iwe imekamilika ,kama itakuwa bado anzeni kimkata fedha, na hii ifanyeni kwa wakandarasi wote nchini ambao wanachelewesha kukamilisha kazi kulingana na mikataba yao,"alisema Chongolo.
Alisema barabara hiyo ni kiunganishi cha huduma kwa wananchi na kutaka ikamilike ndani ya wakati ili wananchi wasiendelee kupata tabu ya usafiri wakati fedha za ujenzi zimeshatolewa.
Akizungumzia barabara hiyo,Mbunge wa Jimbo la Mwanga,Joseph Tadayo(CCM) alisema ujenzi wa barabara hiyo ni ahadi ya rais wa awamu ya nne na hadi sasa bado ujenzi wake unasuasua.
"Hii barabara ni ahadi ya rais wa awamu ya nne,tunaendelea kuisemea hadi ikamilike kwa sababu huku ni eneo la pembezoni na ni mlimani kama isipojengwa na kukamilika wananchi wanaendelea kuteseka,lakini ikikamilika itatusaidia sana kurahisisha usafiri na kupitika nyakati zote,"alisema Tadayo.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni