TET kuandaa Moduli za Mafunzo Kazini Kwa Walimu ili Kuwasaidia Wanafunzi Wasioona
Na Mussa Augustine.
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwabao lengo lake ni kuandaa moduli kwa ajili ya kutolea mafunzo kazini kwa Walimu ili kuongeza umahiri wao katika kuwabaini,kuwachunguza na kutoa afua stahiki kwa wanafunzi wenye changamoto ya kuona.
Hayo yamebainishwa leo Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt Aneth Komba katika mkutano na Waandishi wa Habari kuelezea mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa Mwaka wa fedha 2022/ 2023, ambapo pamoja na mambo mengine amesema kwamba wanafunzi wengi katika shule za awali hadi sekondari wanakumbwa na changamoto ya uoni.
Dkt Aneth amesema kwamba kiasi cha shilingi 82,642,545 zimetengwa kwa ajili ya kuandaa moduli hizo ambapo mkakati huo utasaidia walimu kupata mafunzo kazini namna ya kuwasaidia wanafunzi wengi ambao wanachangamoto ya kutokuona vizuri darasani ,ili waweze kupata elimu bora.
"Utafiti huu wa 2021/22 na 2022/23 tumebaini wanafunzi wengi wanahitimu masomo yao shule za msingi na sekondari wakiwa na ufaulu mbaya,wengine hawajui hata kusoma Wala kuandika,tumefanya utafiti tukabaini kwamba wengi wao wanachangamoto ya uoni lakini kwa kuwaangalia unaweza kudhani wanaona vizuri,hivyo tuta andaa moduli ili kutoa mafunzo kazini kwa walimu ili waweze kuwasaidia watoto wenye changamoto ya aina hiyo" amesema Dkt Aneth.
Aidha amesema pia utafiti mwingine ni ule ambao wanashirikiana na Chuo Kikuu Cha Dar es salaam ,Chuo Kikuu Cha Agakhan, Agakhan foundation (AKF) na EdTech Hub, kufanya utafiti wenye lengo la kubainisha teknolojia ya TEHAMA iliyo nafuu,sahihi na endelevu ya Walimu kazini ili kuboresha matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya elimu ya Msingi kwa shule zilizoko vijijini,ambapo unafadhiliwa na wadau wa maendeleo kwa kiasi cha shilingi 850,000,000.
Kuhusu Mambo mengine yanayotekelezwa na TET ,Mkurugenzi Mkuu Dkt Aneth amesema kwamba kwa Mwaka huu wa fedha 2022/23 TET inaendelea kukamilisha kazi ya usambazaji wa vitabu vya masomo mbalimbali ngazi ya sekondari na kukamilisha uandishi wa vitabu vya masomo mbalimbali kwa kidato cha kwanza hadi saba,ambapo serikali inatumia kiasi cha shilingi 4,238,569,340.00 kuwezesha uandishi na uchapaji wa vitabu vya kiada vya masomo haya kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalumu kuanzia kidato cha kwanza hadi nne.
Hata hivyo amesema pamoja nakuandaa nakala za vitabu hivyo,TET inatambua na kuzingatia umuhimu wa Matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji ,hivyo vitabu vyote vimewekwa katika Maktaba Mtandao inayopatikana katika tovuti ya www.tie.go.tz.,ambapo Maktaba hiyo ina machapisho yote ya kiada na imepakiwa pia machapisho mengine ya ziada yanayoweza kupatikana kwa wanafunzi wanaoona na wasioona.
" Maktaba Mtandao inapatikana bure, TET kwa kushirikiana na UNCEF-Tanzania imebaini makubaliano na kampuni ya simu ya Airtel yanayoruhusu watumiaji wa Maktaba Mtandao kutumia bure Maktaba bila kuwa na kifurushi Cha internet ,TET inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni mengine ya simu ,ninaomba makampuni mengine yajitokeze kwenye eneo hil" ameomba Dkt Aneth
Hakuna maoni
Chapisha Maoni